MAKAMU WA RAIS AIPONGEZA KALIUA KWA KUTUMIA MAPATO YAKE YA NDANI KUPEKA HUDUMA KWA WANANCHI
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua kwa kutumia mapato yake ya ndani kwa ajili ya ujenzi wa muindo mbinu ya afya katika Hospitali na Kituo cha Afya cha Kaliua.
Hatua hiyo itasaidia kusogeza huduma za afya ikiwemo za upasuaji wa mama wajazito na za mama na mtoto karibu na kuwaepusha wananchi kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma hizo katika Wilaya ya Urambo.
Makamu wa Rais alitoa kauli hiyo kwenye mkutano wa hadhara katika uwanja wa Kolimba wilayani Kaliua ikiwa ni siku nne ya ziara yake mkoani Tabora .
Alisema kitendo cha Halmashauri hiyo cha kutenga sehemu ya mapato yake ya ndani kujenga jengo la upasuaji kwenye Kituo cha Afya Kaliua na ununuzi wa vifaa kwa gharama za shilingi milioni 159 na kile cha ujenzi wa jengo la mama na mtoto katika Hospitali ya Wilaya kwa gharama ya milioni 352 ni mfano mzuri ambao unakusudia kusogeza huduma karibu na wananchi.
Makamu wa Rais alizitaka Halmashauri nyingine nazo kutumia sehemu ya mapato yake ya ndani kuboresha huduma za jamii ikiwemo maji , afya , elimu na barabara ili kuwafanya wananchi kuwa na mazingira mazuri katika uzalishaji.
Naye Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) aliziagiza Halmashauri zote nchini kuhakikisha asilimia 60 ya mapato yake ya ndani yanaelekezwa katika shughuli za kujenga miradi ya maendeleo ikiwemo elimu , afya na asilimia 40 ndio itumike katika matumizi mengine.
Alisema Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua imefanya vizuri na kuongeza kuwa ni lazima Halmashauri zote zihakikishe zinatekeleza agizo hilo na zitakazokutwa hazitekelezi watendaji wake watachukuliwa hatua.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua Dkt. John Pima alisema katika mwaka huu wa fedha tayari wametoa mikopo ya shilingi milioni 207 kwa vikundi 61 ikiwa ni sehemu ya asilimia 10 ya mapato yake.
Alisema hadi kufika mwisho wa mwaka wanaweza kutoa mikopo kwa vikundi vingi.
mwisho
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa