MAKAO MAKUU YA HALMASHAURI YA WILAYA YA NZEGA KUJENGA KATIKATI YA NDALA NA PUGE
BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Nzega limependekeza eneo la kujenga makao Makuu yake ambapo liwe katikati ya Kata ya Ndala na Puge.
Hatua hiyo imefikiwa katika kikao cha kawaida cha Robo ya pili cha Baraza la Madiwani baada ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Selemani Sikiete kuwalisha mapendekezo ya wataalamu.
Alisema katika kikao chao walipendekeza Makao Makuu ya Halmashauri yawe Ndala kutokana na eneo hilo kuwa tayari limeshapimwa na kuingizwa katika ramani tayari kwa ujenzi wa Taasisi ikiwemo za Halmashauri.
Sikiete alisema kigezo kingine ni uwepo wa mkongo wa Taifa wa mawasiliano katika eneo hilo ambao unarahisisha shughuli za kimfumo kwa Watendaji na kuongeza kuwa baadhi ya watumishi wameshalipwa fedha za uhamisho kutoka Nzega Mjini kwenda Ndala.
Aliongeza kuwa ujenzi wa makao Makuu ya Halmashauri hiyo mbali na eneo la Ndala utaigharimu fedha nyingi kwa ajili ya kuweka miundo mbinu ya mawasiliano , utayarishaji wa eneo na kulipa tena watumishi stahiki zao za uhamisho.
Baada ya mawasilisho hayo Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Kiwele Bundala aliwahoji Madiwani juu ya pendekezo la Wataalamu ambapo kati ya wote 48 waliunga mkono na mmoja kupinga huko wakipendekeza maboresho.
Diwani wa Kata ya Semembela Fudulu Baya alisema ni vema eneo ambalo itajengwa Ofisi ya Halmashauri ikiwa katikati ya Kata ya Ndala na Puge ili kuwarahisishia wananchi wa Kata nyingine kufika kirahisi kwa ajili ya kuhudumiwa.
Alisema eneo hilo ni vema likawa karibu na barabara ili wananchi wanaposhuka katika vyombo vya usafiri wasitumie gharama nyingine kuelekea katika Ofisi za Halmashauri.
Mwisho
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa