TAARIFA KWA UMMA (PRESS RELEASE) YA
MKUU WA MKOA WA TABORA, MHE. DKT PHILEMON SENGATI
KWA WAANDISHI WA HABARI WA TABORA – TAREHE 04/05/2021,
KUHUSU UZINDUZI WA MWONGOZO WA UWEKEZAJI WA MKOA UTAKAOFANYIKA TAREHE 08 MEI 2021 –
KATIKA UKUMBI WA MTEMI ISIKE MWANAKIYUNGI
Ndugu Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora,
Ndugu Wakuu wa Sehemu na Vitengo Sekretarieti ya Mkoa,
Ndugu zangu Wanahabari,
Mabibi na Mabwana.
Nawasalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Kazi iendelee)
Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema na kutuwezesha kukutana hapa leo kwa lengo la kuwaeleza kuhusu tukio muhimu litakalofanyika Mkoani kwetu tarehe 08/05/2021.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Nichukue nafasi hii kuwataarifu kwamba Mkoa wa Tabora utazindua rasmi Kitabu cha Mwongozo wa Uwekezaji wa Mkoa wa Tabora tarehe 08/05/2021 katika Ukumbi wa Mtemi Isike Mwanakiyungi, uliopo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ambapo, Mgeni Rasmi wa tukio hilo atakuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Geofrey I. Mwambe (Mb).
Ndugu Wanahabari, kwa kuwa ninyi ni wadau muhimu wa maendeleo katika Mkoa wetu, nimeona kuwa ni vema niwaite hapa ili niwafahamishe kuhusu tukio hilo muhimu kwa uchumi wa Mkoa wetu na Taifa kwa ujumla ili nanyi kwa kutumia taaluma yenu mtangaze na kuwahabarisha wananchi wa Mkoa wa Tabora, na Watanzania wote kufuatilia kwa karibu tukio hilo katika vyombo vya habari.
Ndugu Wanahabari, nichukue fursa hii tena, kuwaeleza kwa kifupi umuhimu wa Kitabu cha Mwongozo wa Uwekezaji wa Mkoa wa Tabora. Mwongozo huu unaeleza fursa muhimu zilizopo Tabora ili kumrahisishia mwekezaji kufanya maamuzi ya kuwekeza Tabora, na utamsaidia mwananchi kufahamu jinsi ya kufaidika na uwekezaji tarajiwa. Maeneo muhimu yaliyoainishwa kwenye kitabu cha mwongozo wa uwekezaji ni pamoja na;
Hali ya kijiografia, kisiasa, kijamii, kiuchumi na kiutawala ya Mkoa.
Sababu za kuwekeza Tabora.
Huduma wezeshi zilizopo kwa ajili ya wawekezaji wa ndani na nje ya Mkoa.
Maeneo ya kupaumbele ya kuwekeza katika Mkoa.
Miundombinu wezeshi iliyopo.
Orodha ya taasisi wezeshi zilizopo kwa ajili ya kurahisisha uwekezaji.
Orodha na ukubwa wa Ardhi iliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji mbali mbali na,
Uwepo wa Mawasiliano muhimu (simu & barua pepe) kwa ajili ya kutolea ufafanuzi wawekezaji.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Kauli Mbiu ya Uzinduzi wa Mwongozo wa Uwekezaji wa Mkoa wa Tabora ni: “ Wekeza Tabora kwa Uchumi wa Kijani “ Maana ya kauli mbiu hii ni kuueleza umma kuwa Msingi mkuu wa uchumi wa Tabora unategemea uzalishaji wa malighafi zinazotokana na kilimo, mifugo na maliasili. Hivyo, ni muda muafaka sasa kwa Wananchi wetu kujiandaa na kuzitumia kikamilifu fursa na vivutio vilivyoainishwa katika Mwongozo huo ili kuvutia uwekezaji.
Na kama mnavyofahamu kuwa mnamo 01 Julai, 2020 Nchi yetu iliingia katika uchumi wa kati ambao msingi wake mkuu ni viwanda. Hivyo, nawaomba wananchi wote wa Tanzania kutumia fursa hii kuchangamkia fursa na vivutio vilivyopo katika Mkoa wa Tabora ili kujenga viwanda vya kuchakata na kuongeza thamani ya mazao yatokanayo na kilimo, mifugo, nyuki, madini na maliasili zingine.
Ndugu Wanahabari, hadi kufikia tarehe ya leo, maandalizi ya uzinduzi yanaendelea vizuri, ambapo tumealika wawekezaji wakubwa wa ndani wakiwemo Mohamed Enterprises (MeTL), Azania Group, Bakhresa Group, Kahama Oil Mills na Jambo Group of Companies. Tumewaalika wawekezaji hao ili waje waone fursa zilizopo katika Mkoa wetu na namna watakavyozitumia kufanya uwekezaji mkubwa.
Ndugu Wanahabari,
Ni matarajio yangu kuwa mtausaidia Mkoa wa Tabora kwa kupitia vyombo vya habari kutangaza, kutoa elimu na kuhamasisha wananchi juu ya umuhimu wa Mwongozo wa Uwekezaji ambao utaingizwa katika tovuti ya Mkoa mara baada ya uzinduzi.
WITO WANGU KWA WANANCHI;
Natoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Tabora, taifa kwa ujumla na nchi jirani kujipatia nakala ya kitabu cha mwongozo wa uwekezaji wa Mkoa ambacho kitapatikana bure katika tovuti ya Mkoa wa Tabora mara tu baada ya kuzinduliwa, naomba mkisome kwa makini ili mzielewe fursa na vivutio vya uwekezaji vilivyopo Tabora, kisha mzitumie kuzalisha mali kwa manufaa yenu, Mkoa na Nchi kwa ujumla.
Mwisho, napenda kuwapongeza wanahabari wote wa Mkoa wa Tabora kwa ushiriki wenu katika Kikao hiki kifupi.
Ahsanteni kwa kunisikiliza
…………………………
Dkt Philemon Sengati
MKUU WA MKOA WA TABORA
04.05.2021
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa