MKUU wa Tabora Dkt. Philemon Sengati amewataka Walimu Wakuu kuepuka kujenga makundi miongoni mwa walimu wanaowongoza ili kuwafanya kujiona kitu kimoja na kufanyakazi kwa bidii.
Hatua itasaidia kuwa na ushirikiano ambao utaongeza juhudi katika ufundishaji wanafunzi na kuwawezesha kuongoza katika mitihani mbalimbali ya Kitaifa.
Dkt. Sengati alitoa kauli hiyo mjini Tabora wakati akifungua mkutano wa siku moja wa Chama cha Walimu Wakuu wa Shule Msingi Tanzania(TAPSHA) uliokuwa ukijadili mambo mbalimbali ikiwemo mapambano dhidi ya mimba, utoro, rushwa katika mitihani na mbinu za kuongeza ufaulu kwa wanafunzi katika mitihani ya kitaifa.
Alisema walimu wakuu ni lazima wahakikishe wanaweka mazingira mazuri na kuwaongoza vizuri walimu waliochini yao ili waweze kufanyakazi kwa bidii na moyo wa uzalendo katika kufundisha kwa ajili ya kuongeza ufaulu wa wanafunzi na kuufanya Mkoa wa Tabora kuwa sehemu ya maeneo mengine nchini kuja kujifunza mbinu bora za ufundishaji.
"Hatutasita kuwachukulia hatua walimu wakuu ambao wanawagawa walimu nakusababisha shule zao kuwa na ufaulu hafifu na kuufanya Mkoa kushika namba za chini...Walimu Wakuu wanatakiwa kuwa mfano mzuri wa uongozi kwa waliochini yao, wale watakaoshindwa kuongoza wenzao kwa misingi ya umoja na mshikamano , tutawaondoa katika nafasi zao na kuwapa ambao watatusaidia kuufanya Mkoa wetu uwe darasa" alisitiza
Dkt. Sengati aliwataka Walimu Wakuu kuendelea kuwachukulia hatua kali baadhi ya walimu wasio waadilifu na wenye tabia mbaya za kujihusisha kimapenzi na wanafunzi na hivyo kuwasababishia kurudi nyuma kitaaluma na wengine wao kukatiza masomo kwa kupata ujauzito.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa wa Tabora aliwaagiza Walimu Wakuu kuendelea kusimamia ujenzi wa miundombinu ya shule kwa kusingatia matumizi sahihi ya fedha za umma ili kuondoa tatizo la upungufu katika maeneo yao.
Aliongeza walimu Wakuu wanatakiwa kuendelea kuchukua hatua wazazi wa watoto watoro kwa kushirikiana na viongozi wa Kijiji na Kata kwa kuwafikisha katika vyombo vya Sheria ili kutoa fundisho kwa wazazi wengine wenye tabia za kuacha watoto wao nyumba bila kuwahimiza kwenda Shule.
Awali Katibu Tawala Msaidizi anyeshughulikia Elimu Mkoa wa Tabora Michael Ligola aliwataka Walimu Wakuu kuwa na vipindi katika madarasa yanayokuwa na mitihani ya kitaifa kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za walimu wanaofundisha madarasa hayo na kuwatia moyo wanafunzi ili waweze kusoma kwa bidii na kuweza kufaulu kwa wastani wa juu.
Aliongeza sanjari na ufundishaji ni vema wanafunzi wakapewa mazoezi ya kutosha na mara kwa mara kwa ajili ya kuwajengea uwezo wa kujiamini na kuwa tayari kufanya mitihani mbalimbali ikiwemo ya kitaifa bila woga na hivyo kuweza kufaulu vizuri.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa