RC TABORA AZINDUA MRADI WA UGAWAJI BURE TANI 12,500 ZA MBOLEA KWA WAKULIMA WADOGO NCHINI
MKUU wa Mkoa wa Tabora Dkt. Philemon Sengati amezindua usambazaji mbolea bure unaojulikana kama ‘Action Africa’ ambapo itatoa zaidi ya tani 12,500 za aina ya YaraMila Cereal yenye thamani ya shilingi bilioni 16.5.
Uzinduzi huo umefanyika wilayani Nzega ambapo jumla ya wakulima wadogo 83,000 nchini Tanzania watanufaika kwa kupata mbolea hiyo bila malipo.
Alisema Serikali imeamua kukifanya kilimo kuwa cha kibiashara na kuwaletea maendeleo yao wenyewe na kufurahia shughuli ya kilimo.
Dkt. Sengati alitoa wito kwa wakulima wadogo wanajisajili ili waweze kupata mbolea kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa mahindi na mpunga.
Alisema wakulima ambao watanufaika ma mradi huo wataweza kuongeza uzalishaji wa mahindi katika ekari moja kutoka maguni 2 na kupata magunia 25.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Yara Tanzania Winston Odhiambo alisema chini ya mpango huo, mkulima atahitajika kujisajili kupitia namba *149*46*16# ambapo kitambulisho cha mpigakura na cha taifa kitatumika katika kukamilisha usajili.
Odhiambo alisema lengo la mradi huo ni kukuza uzalishaji wa mahindi na mpunga ili kuhakikisha Tanzania inakuwa na chakula kingi na hivyo kuwa na usalama wa chakula.
Alisema chini ya mpango huo watagawa mifuko mitatu kwa ajili ya ekari moja ya mahindi na mifuko miwili kwa ajili ya ekari moja ya mpunga.
Naye Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe alisema Serikali haitasita kumkamata na kumshitaki kama muhujumu uchumi Msambazaji au mtu atakayekutwa akiuza mbolea hizo ambazo zinapaswa kutolewa bure kwa wakulima wadogo.
Alisema lengo mpango pamoja na kuongeza usalama wa chakula nchini ni pamoja na kuwainua wakulima wadogo ili wakuze kilimo chao kwa nia ya kuwa na uwezo ya kujinunulia mbolea wao wenyewe.
Bashe aliongeza kuwa chini ya mpango huo wakulima pia watapata punguzo la mbegu za mahindi ambapo watanunua kwa shilingi 5500/= badala ya shilingi 12,500/- kwa mfuko wa kilo mbili.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Nzega Advera Bulimba alisema kuwa zaidi ya wakulima wadogo 4000 wameshajisali na wanakusudia kufika wakulima 10,000 wilayani humo
MWISHO
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa