SERIKALI YAENDELEA KUTAFUTA MASOKO YA TUMBAKU
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema Serikali inaendelea kutafuta masoko kwa ajili ya zao la tumbaku nchini ili kuwawezesha wakulima kuzalisha kwa wingi na kuinua kipato.
Ameyasema hayo leo (Jumapili, Julai 14, 2019) wakati akizungumza na wadau wa zao la tumbaku kutoka mikoa mbalimbali. Mkutano huo umefanyika mjini Tabora.
Waziri Mkuu amesema tayari Serikali imeshafanya mazungumzo na nchi mbalimbali zikiwemo za Vietnam na Misri ambayo imeahidi kuisadia Tanzania kupata wanunuzi.
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali inaendelea na mazungumzo na kampuni zinazonunua tumbaku nchini ili ziongeze kiwango cha ununuzi ili kuwawezesha wakulima kuzalisha zaidi.
“Wakulima wanahitaji kuzalisha zaidi lakini wanakwamishwa na kiwango wanachowekewa (ukomo wa uzalishaji) na wanunuzi ambacho ni kidogo ukilinganisha uwezo wa wakulima katika kuzalisha zao hilo.”
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea na mazungumzo na kampuni ya ununuzi wa tumbaku ya Tanzania Leaf Tobacco Company (TLTC) ili iendelee na ununuzi wa zao hilo.
Amesema awali kampuni ya TLTC ambayo ilikuwa ni miongoni mwa wanunuzi wa tumbaku nchini ilitoa kusudio la kutaka kuacha kununua zao hilo.
Pia, Waziri Mkuu amesema Serikali inashirikiana na nchi ya Malawi katika utafutaji wa masoko ya zao hilo na tayari kampuni za Malawi zimeahidi kununua tumbaku nchini.
Amesema hayo ni miongoni mwa mafanikio ya ziara aliyoifanya Rais, Dkt. John Magufuli aliyoifanya hivi karibuni nchini Malawi. Amewataka wakulima waendelee kuwa na subra.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa