TAASISI ZA UMMA MKOANI TABORA ZINADAIWA ZAIDI YA BILIONI 1.8 ZA BILI ZA MAJI
MAMLAKA tatu za Maji safi na Usafi wa Mazingira Mkoani Tabora zinadaia taasisi mbalimbali za umma bili ya huduma ya maji ya zaidi ya shilingi bilioni 1.8.
Kauli hiyo imetolewa na Wakurugenzi Watendaji wa Mamlaka za Maji za Tabora , Nzega na Igunga wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt Philemon Sengati ya kukagua mradi wa kutoa maji ziwa Victoria kwenda Mkoani humo.
Mkurugenzi Mtendaji wa TUWASA Joel Rugemalila alisema kwa uapnde wao wanazidai Taasisi za Umma kiasi cha shilingi bilioni 1.7 ikiwa ni malimbikio ya madai ya madeni ya bili za maji za mwaka wa fedha wa 2017/18, 2018/19 na 2019/20.
Alisema miongoni mwa wadai ni pamoja na Jeshi, Magereza , Polisi na Hospitali
Rugemalila alisema makusanyo halisi ya TUWASA kwa mwezi yatakiwa kuwa zaidi ya shilingi milioni 450 lakini kutokana na Taasisi hizo kutolipwa kwa madeni ya maji wamekuwa wakishuka katika ukusanyaji na kupata kiasi cha milioni 350 kwa mwezi.
Alisema hali hiyoimesababisha kuwepo ugumu wa uendshaji wa Mamlaka hiyo kwa kuwa inahitaji shilingi milioni 90 za umeme na shilingi milioni 60 za kununulia dawa za kusafisha maji.
Mkurugenzi huyo Mtendaji wa UWASA aliongeza kuwa wamekuwa wakitoa kiasi cha milioni 145, kulipa mishahara ya watumishi na shilingi milioni 64 kulipa Mamlaka ya Maji ya Kahama Shinyanga (KASHUWASA) ikiwa ni malipo ya maji wanayonunua kutoka kwao ili kuwasambazia wateja.
Rugemalila alisema wangekuwa wakilipwa fedha hizo zingesaidia sana kuboresha huduma za upatikanaji wa maji kwa wananchi kwa wakati kwa kuongeza mitandao ya maji katika maeneo yote ambayo hayajafikiwa.
Kwa upande wa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamalaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira katika Mji wa Nzega Lightness Gai alisema wanadai Taasisi mbalimbali za Serikali jumla ya shilingi milioni 43.9.
Alisema wamekuwa wakifuailia lakini kasi ya ulipaji umekuwa mdogo jambo ambalo limesababisha kupungukiwa fedha kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya zamani ya kusafirishia maji.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Igunga (IGUWASA) Athuman Kiludumya alisema wanadai Taasisi za umma zaidi ya shilingi milioni 56.1.
Alisema Taasisi wanazidai ni Magereza, Polisi na Hospitali ya Wilaya.
Kufuatia hali, Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Sengati ameziagiza Mamlaka zote tatu za utoaji wa huduma ya majisafi na usafi wa mazingira kuhakikisha zinampelekea orodha ya wadaiwa na kiasi ili aweze kukutana nazo.
Alisema anataka kukutana nazo ili ziweze kuonyesha mpango wao wa kulipa madeni yao ili fedha zitakazopatikana ziweze kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wale wote ambao hawajafikiwa na huduma hiyo.
Mwisho
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa