WAKAZI WA IGUNGA WATAKIWA KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIA NCHI
SERIKALI Mkoani Tabora imewataka wakazi wa Igunga kutumia mafunzo mbalimbali wakati wa utekelezaji wa Mradi Shirikishi wa kukabiliana na Mabadiliko ya Tabia Nchi Igunga (Igunga ECO – Village) katika kuhakikisha waendelea kufanya shughuli ambazo ni rafiki wa mazingira ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi
Kauli hiyo imetolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri wakati wa sherehe za kufunga Mradi Shirikishi wa kukabiliana na Mabadiliko ya Tabia Nchi wa Igunga.
Alisema wakiendelea kuzingitia mafunzo waliyopata wataendelea kuwa na uhakika wa chakula wakati wote na kukabiliana na magonjwa mbalimbali ambayo yanatokana na ukosefu wa vyoo safi na salama hasa yale ya mlipuko.
Mwanri alisema kuwa katika kipindi cha minne mradi huo ambao umetumia zaidi ya shilingi bilioni 5 umeweza kutekelezaji shughuli mbalimbali zinahusika na upunguzaji wa athari zamazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Alizitaja shughuli zilizofanyika ni pamoja na kuwaelimisha wakulima kuongeza uzalishaji mazao . upandaji wa miti, ujenzi wa majiko banifu, uvunaji wa maji ya mfua, ujenzi wa vyoo vya kisasa na ufugaji wa kuku, samaki na ng’ombe.
Mwanri aliutaka uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga kuhakikisha unaendeleza mafunzo hayo katika Kata zote za Wilaya hiyo ili wananchi wengi waweze kupata elimu ya ulizashaji wa mazao ambao ni rafiki na mazingira kwa ajili ya kuwa na chakula kiingi wakati wote.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Wakulima wa Kata ya Mbutu na Igunga waliokuwa wakinufaika na mradi wa Igunga Eco Village Mathias Luhende alisema baada ya mafunzo wakulima wa eneo husika wametambua mbinu za kilimo na uvuvi ambao ni rafiki na mazingira.
Alisema pia wameweza kuboresha utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti, usafi wa mazingira kuanzia ngazi za kaya zao, shule na katika Taasisi za dini kwa kuimarisha ujenzi wa vyoo vya kisasa.
Luhende aliongeza kuwa wamepunguza tatizo la upatikanaji wa maji kwa kujifunza teknolojia ya uvunaji wa maji na uchimbaji wa visima na matumizi ya chujio la maji ambalo limepunguza magonjwa la mlipuko kwenye eneo la mradi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Revoctaus Kuuli alisema mradi huo umesaidia kutoa elimu mbalimbali ikiwemo ufugaji wa samaki ambapo kwa kipindi cha miaka minne cha utekelezaji umeweza kutoa jumla ya vifaranga 90,000 vya samaki ili kuwawezesha kujiongezea kupato na kuepuka kufanya shughuli zinaharibu mazingira.
Alisema kupitia mradi huo wakazi wa Kata hizo wameweza kuunda na kuanzisha Kamati 49 za usafi na mazingira kwa ajili ya ufuatiliaji wa usafi ngazi ya kaya ili kuikinga jamii na magonjwa ya mlipuko.
Kuuli alisema katika kipindi cha miaka minne ya utekelezaji wa mradi huo jumla ya sola 600 zimetolewa kwa kwa wanafunzi na wakulima na kupata mafunzo ya utengenezaji wa majiko banifu ambapo majiko 58 yalitengenezwa.
Mradi huu ulianza kutekelezwa katika Kata za Mbutu na Igunga wilayani Igunga 2015 na ulihusu sekta za Mazingira na Maliasili, Maji, Kilimo na Uvuvi na Maendeleo ya Jamii .
Mradi huu ulikuwa ukifadhiliwa na Umoja wa Nchi za Jumuiya ya Ulaya ,Shirika la Mitamba Uholanzi (Heifer Nederland), Shirika la Mitamba (HEIFER Tanzania), Shirika la Kimataifa la Utafiti wa Fiziolojia ya Wadudu na Mazingira (ICIPE), Maji kwa wote( Aqua for All ) kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Igunga.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa