Mkuu wa Wilaya ya Sikonge, Mhe. Cornel Lucas Magembe, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Paul Chacha, ameongoza kikao cha tathmini ya mkataba wa lishe katika ngazi ya mkoa, kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Isike Mwanakiyungi.
Katika ufunguzi wa kikao hicho, Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Dkt. John Mboya, alizipongeza halmashauri zilizotekeleza afua za lishe kwa ufanisi na kufikia alama ya kijani. Hata hivyo, alibainisha kuwa bado kuna changamoto chache katika masuala ya lishe,ikiwemo udumavu, utapiamlo, na changamoto za afya ya uzazi. Alisisitiza kuwa kila kiongozi anapaswa kutimiza wajibu wake kwa ubunifu ili kuhakikisha afua za lishe zinatekelezwa kwa ufanisi zaidi.
Aidha, Dkt. Mboya aliwataka wataalam wa halmashauri kusimamia kwa umakini suala la usafi wa mazingira, akibainisha kuwa mazingira safi ni msingi wa afya bora. Alionya kuwa uchafu wa mazingira unasababisha magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu, hivyo ni muhimu kwa wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri kushirikiana kusimamia usafi kwa kutumia sheria ndogo za mamlaka za serikali za mitaa.
Kwa upande wake, Mhe. Magembe alitoa maelekezo kwa wataalam wa halmashauri kuhakikisha shule za msingi na sekondari, zahanati, na vituo vya afya vinatoa chakula chenye lishe bora. Pia, alisisitiza upandaji wa miti ya matunda katika taasisi hizo ili kuongeza upatikanaji wa lishe bora kwa wanafunzi pamoja na wananchi wanaofika hospitali kupata huduma za afya.
Katika hatua nyingine, alihimiza uhamasishaji wa wananchi kujenga vyoo bora kwa gharama nafuu ili kuondokana na magonjwa ya mlipuko.
Kikao hicho kilihitimishwa kwa maazimio kadhaa muhimu, ikiwemo kuhakikisha wakurugenzi wa halmashauri wanasimamia vyema utoaji wa fedha kwa ajili ya upatikanaji wa chakula shuleni, ujenzi wa vyoo bora, na kuandaa mkakati maalum wa upandaji wa miti ya matunda na bustani za mboga shuleni. Pia, ilisisitizwa utoaji wa elimu kuhusu malezi bora na maadili kwa watoto, pamoja na juhudi za kuzuia vitendo va ukatili kwa watoto na ndoa za utotoni.
Mwisho
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa