Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko, amepongeza juhudi za Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na kampuni tanzu ya ETDCO kwa kazi kubwa na ya mfano waliyoifanya katika kuboresha huduma ya umeme wilayani Urambo, mkoani Tabora.
Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo cha kupokea, kupoza na kusambaza umeme cha Uhuru chenye uwezo wa kilovoti 132/33, Dkt. Biteko alisema mradi huo ni mfano wa utekelezaji bora unaoonesha matokeo ya dhahiri kwa wananchi.
“ETDCO na TANESCO mmefanya kazi ya mfano. Mmeonesha kuwa kazi inazungumza zaidi kuliko maneno. Mradi huu utaiwezesha Tabora kuwa kitovu cha umeme kwa mikoa ya Tabora na Katavi,” alisema Dkt. Biteko huku akiwataka wananchi kuthamini juhudi hizi za serikali.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Paul Chacha, alimshukuru Waziri Biteko kwa mchango wake mkubwa katika kusukuma mbele miradi ya nishati, akisisitiza kuwa kituo hicho kimewezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa wananchi wa Urambo na maeneo jirani. “Mradi huu ni chachu ya maendeleo. Umeme sasa unapatikana kwa uhakika na tunatarajia kuzalisha hata ziada itakayoweza kuuzwa nje ya nchi,” alisema Chacha.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora, Ndg. Said Nkumba, alimpongeza Dkt. Biteko kwa mageuzi chanya katika sekta ya nishati, na kuahidi kuwa kuelekea uchaguzi wa 2025, chama hicho kitawasimamisha wagombea makini na wanaokubalika na wananchi.
Kwa upande wake, Mbunge wa Urambo, Mhe. Magreth Simwanza Sitta, alieleza furaha yake kwa kufanikishwa kwa usambazaji wa umeme katika vijiji vyote 59 na vitongoji 136 vya wilaya hiyo. Hata hivyo, aliwasilisha ombi kwa serikali kuangalia upya gharama za kuunganishiwa umeme, pamoja na kuhakikisha vitongoji 126 vilivyobaki vinapatiwa huduma hiyo.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Bi. Renata Ndege, alisema mradi huo una vipengele viwili muhimu: ujenzi wa njia ya umeme yenye urefu wa kilomita 115 kutoka Tabora hadi Urambo, na ujenzi wa kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Uhuru. Alieleza kuwa wananchi wote waliopitiwa na mradi huo walishalipwa fidia kwa mujibu wa sheria.
Dkt. Biteko aliwatoa hofu wananchi kuwa serikali inaendelea na jitihada za kuhakikisha umeme unamfikia kila Mtanzania, huku akifikisha salamu za upendo na pongezi kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. “Mama Samia anawapenda na anatambua juhudi za watu wa Tabora katika kulitumikia taifa,” alisema.
Kuhusu uchaguzi mkuu ujao, Dkt. Biteko alisema: “Tutagawanyika makundi mawili—watasema tutafanya na wale watakaosema tumefanya. Msikilizeni yule mwenye ushahidi wa kazi mkononi. Mama Samia ana yakuonesha. Mama Sitta ana yakuonesha.”
Mradi huo mkubwa wa miundombinu ya umeme unakadiriwa kugharimu shilingi bilioni 44 na unatarajiwa kuwa chachu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wilaya za Urambo, Sikonge, Kaliua na mikoa ya Tabora na Katavi kwa ujumla.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa