Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Dkt. John Mboya, amefanya ziara ya kukagua hali ya maeneo ya kata za Mwinyi na Malolo yaliyoathiriwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua za masika zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumza na wananchi pamoja na viongozi wa kata ya Malolo, Dkt. Mboya amepongeza uongozi wa Manispaa ya Tabora ukiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji pamoja na Mstahiki Meya kwa kuchukua hatua za haraka kushughulikia athari za mafuriko hayo, hatua zilizosaidia kunusuru makazi ya wananchi na kuimarisha usalama wao.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari kubwa katika kulinda usalama wa maisha na mali zao, hususan katika kipindi hiki ambacho mvua za masika zinaendelea kunyesha nchini. Vilevile, amewakumbusha viongozi wa mamlaka za serikali za mitaa kusimamia kikamilifu utekelezaji wa sheria, taratibu na kanuni za ujenzi, akisisitiza umuhimu wa kuepuka utoaji wa vibali vya ujenzi katika maeneo hatarishi yanayotuamisha maji.
Akieleza chanzo cha mafuriko, Kaimu Meneja wa TARURA Mkoa wa Tabora, Mhandisi Subira Manyama, amesema mvua kubwa ilisababisha maji kukosa njia za kupita kutokana na barabara kuwa bado katika hatua za ukamilishaji na hivyo kuingia kwenye makazi ya wananchi. Ameeleza kuwa TARURA tayari imeanza kukamilisha mitaro na kujenga njia za muda mfupi, huku kazi hiyo ikitarajiwa kukamilika ndani ya siku mbili.
Kwa upande wao, viongozi wa kata hizo pamoja na wananchi wameishukuru Serikali kwa hatua za haraka zilizochukuliwa kukabiliana na athari za mafuriko, wakieleza kuwa jitihada hizo zimeongeza imani ya wananchi na kuimarisha ushirikiano kati ya jamii na serikali katika nyakati za dharura.
Katika hatua nyingine, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Tabora, Afande Laizer, amesema jeshi hilo lipo tayari kutoa huduma za uokozi muda wote. Amewahimiza wananchi kutoa taarifa mapema pindi yanapotokea maafa yanayotokana na mvua, kwa kutumia namba ya dharura ya bure 114, ili hatua stahiki zichukuliwe kwa wakati.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa