Na. Ofisi ya mkuu wa mkoa wa Tabora.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Dkt. John Mboya, ametoa pongezi kwa kampuni ya HolyKitchen Tanzania Co. Ltd kwa kutwaa tuzo katika hafla ya tano ya utoaji wa Tuzo za Wanawake Wenye Viwanda nchini, iliyofanyika Machi 26, 2025 katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.
Akizungumza ofisini kwake wakati akipokea ugeni kutoka kwa wajasiriamali hao, Dkt. Mboya aliwapongeza kwa ubunifu na juhudi zao zilizozaa matunda ya ushindi. Alisema ushindi huo ni heshima kubwa kwa Mkoa wa Tabora na unatoa motisha kwa wajasiriamali wengine kuendelea kuongeza bidii.
“Hii ni ishara kwamba Tabora tunayo hazina ya wajasiriamali wabunifu na wachapakazi. Serikali inaendelea kuunga mkono juhudi hizi kupitia mikopo isiyo na riba ya asilimia 10 inayotolewa kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu,” alisema Dkt. Mboya.
HolyKitchen Co. Ltd ni kampuni inayojishughulisha na mnyororo wa thamani wa uchakataji wa mazao ya maziwa. Kupitia mafanikio yao, waliwasili ofisini kwa Mkuu wa Mkoa kutoa shukrani kwa serikali kwa kuwawezesha kupitia mikopo isiyo na riba pamoja na kutambulisha tuzo waliyotwaa kwa uongozi wa mkoa.
Ugeni huo uliongozwa na Mkurugenzi wa Bodi ya Tanzania Women’s Chamber of Commerce (TWCC) Kanda ya Kati, Bi. Lucy Mtinya, akifuatana na Mwenyekiti wa TWCC Mkoa wa Tabora, Bi. Teresia Mzobora. Pia walikuwepo wanachama wa TWCC akiwemo Bi. Fatuma Kisanji pamoja na Bi. Winfrida Mkombe ambaye ndiye mshindi wa tuzo hiyo.
Tuzo hizo hutolewa kwa kutambua mchango wa wanawake katika sekta ya viwanda na biashara, ambapo kwa mwaka huu mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Jaffo.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa