Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mh.Balozi Dkt. Batilda Salha Burian leo tarehe 24/04/2023 amezindua miradi mitatu ya maji wilayani Igunga. Ambapo miradi hiyo mitatu ni sehemu ya miradi saba yenye thamani ya shilingi Bilioni 2.3 ambayo itakwenda kuhudumia wananchi wapatao 41,951. Amewataka wananchi kutambua juhudi za serikali katika kuboresha huduma za maji vijijini. Na hivyo amewaomba wananchi wa Igunga kulinda miundombinu ya maji pamoja na kuhifadhi vyanzo vya maji kupitia zoezi la upandaji wa miti. Na pia amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuleta miradi mingi ya maji mkoani Tabora.
Akisoma taarifa ya miradi, Meneja wa RUWASA (W) Igunga Muhandisi Marwa Sebastian Muraza amebainisha kuwa, miradi hiyo saba imekamilika kwa asilimia mia moja na tayari iko tayari kwa matumizi. Ametoa pongezi na shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan, ambapo kupitia wizara ya maji, wilaya ya Igunga imepata fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maji.
Nao baadhi ya wananchi wanaofaidika na miradi hiyo, wameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kusogeza huduma bora ya maji vijijini, na kwamba sasa watatumia muda wao katika shughuli za kiuchumi badala ya kutumia muda huo kutafuta maji umbali wa zaidi kilometa tano.
Uzinduzi wa miradi hiyo saba ni sehemu ya mIradi ya maji 57, ambayo RUWASA mkoa wa Tabora hadi kufikia mwezi Machi, 2023 itakuwa imeitekeleza, yenye thamani ya Tshs. Bilioni 61.1 ambapo miradi 46 yenye thamani ya Tshs. Bilioni 54.5 inatekelezwa na wakandarasi na miradi 11 yenye thamani ya Tshs. Bilioni 6.6inatekelezwa na wataalam wa ndani (Force Account).
____________________
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa