Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Dkt. John Mboya, ameongoza uzinduzi wa mradi wa kupambana na ugonjwa wa selimundu (Sickle Care) katika ukumbi wa mikutano wa Isike, Mwanakiyungi. Zoezi hili linatokea katika wakati muhimu ambapo mkoa wa Tabora umeendelea kuwa na kiwango kikubwa cha wagonjwa wa ugonjwa huu.
Akitoa taarifa kuhusu hali ya ugonjwa wa selimundu mkoani Tabora, Katibu Tawala Msaidizi wa Afya, Dkt. Honoratha Rutanisibwa, alieleza kuwa selimundu ni ugonjwa wa kurithi unaoathiri seli nyekundu za damu. Alisema kuwa mkoa wa Tabora ni miongoni mwa mikoa nchini yenye kiwango kikubwa cha wagonjwa, ambapo mwaka 2023 mkoa huu ulikuwa na wagonjwa 6,384, na mwaka 2024 idadi ya wagonjwa iliongezeka hadi kufikia 8,465.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Melian Foundation, Bw. Samwel Mabewa, aliishukuru serikali kwa ushirikiano mkubwa kutoka kwa Wizara ya Afya, TAMISEMI, pamoja na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora kwa ushirikiano walioupata na kuwa umeongeza ufanisi katika kupambana na ugonjwa wa selimundu.
Mradi wa Sickle Care, una lengo la kutoa elimu sahihi kuhusu ugonjwa wa selimundu, ili wananchi waweze kuelewa na kutouhusianisha na imani za kishirikina. Aidha, mradi huu utawezesha upimaji na utambuzi wa mapema wa ugonjwa wa selimundu kwa watoto chini ya miaka mitano, jambo litakalosaidia kutibu ugonjwa huu kwa urahisi. Vilevile, mradi huu utatoa mafunzo kwa wahudumu wa afya ili waweze kumudu vizuri katika kukabiliana na ugonjwa wa selimundu katika maeneo yao.
Afisa kutoka Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Bw. Kalidushi Charles, alitoa rai kwa mamlaka za serikali za mitaa kuongeza juhudi katika kupambana na ugonjwa huu kwa kutenga bajeti ya kusaidia juhudi za serikali na wadau katika kupambana na ugonjwa wa selimundu.
Dkt. Hamad Nyembea, Mkurugenzi wa Huduma za Tiba kutoka Wizara ya Afya, alieleza kuwa wizara hiyo ina mikakati madhubuti ya kinga na tiba dhidi ya ugonjwa wa selimundu, ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa umma, kuwahamasisha wananchi kupima na kujua hali zao, na kuanza matibabu mapema, hasa kutokana na ongezeko kubwa la ugonjwa huu kwa miaka ya hivi karibuni.
Akizungumza katika uzinduzi wa huduma hiyo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Dkt. John Mboya, alisisitiza umuhimu wa waganga wakuu wa halmashauri kusimamia mradi huu kwa umakini, ili utekelezwe kwa ufanisi mkubwa na kuleta matokeo chanya katika kupunguza athari za ugonjwa wa selimundu. Aliongeza kuwa ni muhimu kutoa elimu kwa wananchi kuhusu ugonjwa huu na hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kudhibiti ugonjwa wa selimundu.
Dkt. Mboya alihitimisha zoezi la uzinduzi kwa kugawa vifaa kwa wataalam wa afya, ikiwa ni pamoja na dawa na mashine za kuthibitisha uwepo wa ugonjwa huo. Mradi huu wa Sickle Care unadhaminiwa na shirika lisilokuwa la kiserikali la Melian Foundation kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Afya. Zoezi hili la uzinduzi linatarajiwa kuwa na manufaa makubwa kwa jamii ya mkoa wa Tabora na kusaidia katika juhudi za kupambana na ugonjwa wa selimundu nchini.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa