Tabora,Tarehe 1 Machi , 2025.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Dkt. John Rogath Mboya, leo amefanya mkutano na waandishi wa habari ofisini kwake, akitoa maelezo muhimu kuhusu maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake, ambayo huadhimishwa kila mwaka tarehe 8 Machi.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Mhe. Dkt. Mboya alisisitiza umuhimu wa kuungana pamoja kama jamii katika kutetea haki za wanawake na wasichana, na kuhakikisha kuwa kila aina ya vikwazo vinavyowazuia wanawake kujikwamua kiuchumi na kufikia usawa vinatokomezwa. Alisema kuwa hilo ni jukumu letu sote, kwa kuzingatia makubaliano ya sheria za kimataifa zinazotetea haki za wanawake.
Dkt. Mboya alieleza changamoto kubwa inayozorotesha maendeleo ya wanawake na watoto wa kike mkoani Tabora, akitaja mimba za utotoni,mila na desturi potofu zinazokandamiza wanawake katika jamii nyingi za Kiafrika kama kikwazo kikubwa. Alitoa wito kwa jamii kushirikiana ili kumaliza changamoto hizi na kuimarisha hali ya maisha ya wanawake na wasichana katika mkoa wa Tabora.
Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake kwa mwaka huu 2025 yatafanyika kitaifa mkoani Arusha, ambapo mgeni rasmi atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan. Aidha, maadhimisho ya kikanda yatafanyika mkoani Kigoma, na mgeni rasmi katika maadhimisho hayo atakuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango.
Kimkoa, maadhimisho haya yatafanyika katika Halmashauri ya Mji wa Nzega, katika uwanja wa Samora na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mhe. Paul Matiko Chacha,Mkuu wa mkoa wa Tabora.
Dkt.Mboya ametoa wito kwa wananchi wote kujitokeza kwa wingi katika maadhimisho haya, na ameelekeza mamlaka ya serikali kuanzia ngazi ya kijiji, kata, wilaya, na mkoa kufanya maandalizi ya maadhimisho haya, kwa lengo la kuonesha hali halisi ya mapambano na mafanikio ya ukombozi wa wanawake na wasichana katika jamii.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake kwa mwaka 2025 ni: "Wanawake na Wasichana Mwaka 2025: Tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji!"
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa