Kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Tabora, Mhe. Gulamhussein Dewji, akiambatana na viongozi mbalimbali kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, ametembelea Kituo cha Nyumba ya Huruma cha Mama Teresa kilichopo Kata ya Kanyenye, Manispaa ya Tabora.
Katika ziara hiyo, Mhe. Dewji na ujumbe wake walitembelea makundi mbalimbali yanayohudumiwa katika kituo hicho, yakiwemo makundi ya wazee, watu wenye ulemavu pamoja na watoto wanaoishi katika mazingira ya uhitaji, ili kujionea hali zao na namna huduma za malezi na ustawi zinavyotolewa.
Akizungumza wakati wa kukabidhi mahitaji mbalimbali ya kijamii, yakiwemo mchele, unga, mafuta ya kupikia, sabuni pamoja na vinywaji, Mhe. Dewji amewapongeza Masista wa kituo hicho kwa moyo wao wa upendo, kujitoa na kujali makundi ya wahitaji, akieleza kuwa huduma wanazotoa ni kielelezo cha utu na mshikamano wa kijamii. Aidha, amepongeza mazingira mazuri ya kituo hicho pamoja na kazi kubwa inayofanyika katika kuwahudumia wahitaji.
Kwa upande wake, Sister Maria Rozalia, akizungumza kwa niaba ya uongozi wa Kituo cha Nyumba ya Huruma cha Mama Teresa, ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushirikiano na msaada unaoendelea kutolewa, hususan huduma bora za afya wanazozipata kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora – Kitete pale zinapohitajika.
Vilevile, Sister Maria ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Tabora na maeneo ya jirani kufika katika kituo hicho kuwatembelea wahitaji, akibainisha kuwa mahudhurio hayo huwapa faraja kubwa, moyo wa matumaini na kuwafanya wajisikie kuthaminiwa katika jamii.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa