Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Paulo Chacha ameiongoza Kamati ya Usalama ya Mkoa kukagua mradi wa ujenzi wa Soko Kuu la Manispaa ya Tabora, unaotekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 19.9 kwa ufadhili wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia mkopo wa Benki ya Dunia.
Katika ukaguzi huo, ilibainika kuwa mradi umekumbwa na ucheleweshaji kutokana na kugundulika kwa maji mengi kwenye udongo katika kina kifupi cha ardhi, hali iliyohitaji marekebisho ya usanifu wa msingi ili kuhakikisha uimara wa majengo.
Wakati wa tathmini ya taarifa za utekelezaji, Mhe. Chacha alipokea maelezo yanayohusu madai ya matumizi mabaya ya fedha za mradi. Taarifa hizo zilitokana na mawasiliano rasmi kati ya mkandarasi na meneja wa mradi, Mhandisi Francis Mwakajinga, ambapo ilidaiwa kuwepo kwa matumizi yasiyo sahihi ya fedha. Meneja huyo alithibitisha kuwepo kwa matumizi hayo ambayo yanakadiriwa kufikia shilingi milioni 117.
Mhe. Chacha ameonesha kuchukizwa na vitendo vya aina hiyo, na ameeleza kuwa vitendo hivyo vinakinzana na sheria na vinaathiri juhudi za serikali katika kuharakisha maendeleo kwa wananchi. Ameagiza Jeshi la Polisi kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa taratibu za kisheria pamoja na kumundoa Mhandisi huyo katika kazi ya kusimamia mradi huo.
Mradi wa Soko Kuu la Tabora ni miongoni mwa miradi mikubwa chini ya mpango wa Uboreshaji Miundombinu Shindanishi katika Miji (TACTIC) na ni sehemu ya ahadi iliyotolewa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa wananchi wa Tabora katika kuelekea kukamilisha miundombinu inayochochea huduma na uchumi wa eneo hilo.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa