Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Paulo Chacha, amefungua rasmi Mkutano Mkuu wa siku mbili wa Umoja wa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi Tanzania Bara (TAPSHA) ngazi ya mkoa, uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa shule ya sekondaro Themi Hill, mjini Tabora. Mkutano huo umebeba umuhimu mkubwa katika kuboresha uongozi wa elimu na kuimarisha ushirikiano miongoni mwa walimu wakuu.
Akizungumza wakati wa utangulizi, Mwenyekiti wa TAPSHA Mkoa wa Tabora, Iddy Gunto, alisema umoja huo umeanzishwa ili kuwaunganisha walimu wakuu wote wa shule za msingi nchini. Alibainisha kuwa kupitia TAPSHA, mkoa umeimarisha usimamizi wa taaluma na kuongeza ufaulu, hali iliyofanya Tabora kushika nafasi ya 16 kitaifa kwa asilimia 81.1. Aliongeza kuwa wanamshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kulindaa maslahi ya walimu, ikiwa ni pamoja na upandishaji vyeo na stahiki zingine.
Kwa upande wake, Afisa Elimu Mkoa wa Tabora, Mwl. Upendo Rweyemamu, alisema mkutano huo unalenga kufanya tathmini ya utekelezaji shughuli za taaluma shuleni kwa mwaka 2025 na kuweka mikakati ya pamoja ili kuboresha ufaulu kwa mwaka wa masomo 2026. Aidha alisisitiza kuwa mkutano huo utawajengea uwezo walimu wakuu katika maeneo ya udhibiti ubora pamoja na masuala yanayohusiana na Tume ya Utumishi wa Walimu.
Kwa upande wake,Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Dkt. John Mboya, amewapongeza walimu na wazazi kwa ushirikiano uliowezesha mkoa kupata matokeo mazuri kitaifa. Aliwataka walimu wakuu kuimarisha mahusiano na wazazi, kuhakikisha upatikanaji wa chakula shuleni, na kujenga mawasiliano yenye staha baina ya walimu na viongozi wao, akisisitiza kuwa motisha na mazingira bora ya kufundishia ni nguzo muhimu za ufaulu.
Akiwahutubia maelfu ya walimu wakuu pamoja na viongozi wa elimu ngazi ya mkoa na wilaya, Mgeni Rasmi Mhe. Chacha aliwahimiza walimu wakuu kuendeleza umoja wao kwa weledi. Alikabidhi mchango wa shilingi milioni 10 kwa TAPSHA ili kuimarisha mfuko wa umoja huo, huku akiwahimiza watumishi kujiendeleza kielimu. Alisisitiza kuwa umahiri katika utendaji hutokana na kuongeza ujuzi, kusoma na kufanya utafiti wa mara kwa mara, sambamba na kujituma katika majukumu ya kila siku.
Mkutano huo ulihusisha walimu wakuu wote wa shule za msingi mkoa wa Tabora pamoja na maafisa elimu kata, ukiwa chini ya kaulimbiu “Matokeo Bora 2026, Inawezekana – Timiza Wajibu Wako.” Kaulimbiu hiyo inalenga kuongeza ufanisi wa sekta ya elimu na kuhimiza uwajibikaji katika ngazi zote.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa