MHE. CHACHA AONGOZA MAADHIMISHO YA SIKU YA MAZINGIRA DUNIANI WILAYANI URAMBO: KWA KUFANYA USAFI, KUPANDA MITI NA KUTOA WITO WA KUTUNZA MAZINGIRA.
Na. Robert Magaka – Urambo, Tabora.
Katika kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Paulo Chacha, ameongoza mamia ya wananchi wa Mkoa wa Tabora kushiriki katika shughuli za usafi na upandaji miti katika stendi kuu ya mabasi ya wilaya ya Urambo, ikiwa ni sehemu ya kuhimiza ulinzi na uhifadhi wa mazingira.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Urambo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kaliua, Ndugu Raymond Mweli, aliwapongeza watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora pamoja na watendaji wa wilaya zote kwa kuendeleza utekelezaji wa sera ya taifa ya uhifadhi wa mazingira.
“Hakuna maendeleo,hakuna maisha bora bila kuwa na afya bora, ni wajibu wetu sisi sote,kuendelea kuhifadhi mazingira yetu,kuhakikisha tunaelimishana juu ya umuhimu wa kuendelea kuhifadhi mazingira yetu.” alisema Mweli.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Urambo, Mhe. Margareth Sitta, aliwashukuru wananchi kwa ushirikiano wao. Pia aliiomba serikali kupitia TANROADS kuunganisha kwa kiwango cha lami kipande cha barabara kinachotoka stendi hadi barabara kuu ya Kaliua ili kuwezesha mabasi kufika stendi kwa urahisi zaidi na kuongeza mapato ya halmashauri.
Akihutubia hadhira hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Paul Chacha aliwataka wananchi kuendelea kushiriki katika jitihada za kuhifadhi mazingira huku akisisitiza kuwa mazingira safi na salama ni msingi wa maendeleo endelevu.
"Napenda mtambue kwamba matumizi ya kuni na mkaa hapa nchini Tanzania yanaathiri sana hali ya misitu yetu.,Hali hii inachangia uharibifu wa ardhi pamoja na vyanzo vya maji hivyo tunapaswa kutumia nishati safi ya kupikia ili kupunguza athari katika misitu na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi" alisisitiza Mhe. Chacha.
Katika hatua nyingine, Mhe. Chacha aliipongeza Wilaya ya Sikonge kwa kupiga hatua kubwa katika maandalizi ya biashara ya hewa ya ukaa, akibainisha kuwa kila wilaya ya mkoa wa Tabora inapaswa kuwa na mpango huo ili kuchangia uchumi wa taifa na kuhifadhi mazingira.
Aidha, aliiagiza TANROADS kushughulikia suala la barabara ya kuingia stendi ya Urambo kama jambo hilo lilivyoelezwa na Mhe. Sitta, pamoja na halmashauri kuangalia upya viwango vya upangishaji wa vibanda vya biashara ili viwe rafiki kwa wananchi wa kipato cha chini.
Katika kumaliza hotuba yake, Mhe. Chacha alitumia nafasi hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uongozi thabiti unaoendelea kuwaletea maendeleo Watanzania, akisema wananchi wa Tabora ni mashahidi wa mageuzi makubwa yanayofanyika nchini.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa