Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Paulo Chacha, amepokea ugeni kutoka Kampuni ya United Capital Fertilizer of Zambia ya nchini Zambia ambao wameonesha nia thabiti ya kuwekeza nchini Tanzania kwa kujenga kiwanda kikubwa cha mbolea katika Mkoa wa Tabora.
Ugeni huo, ukiwa katika ziara ya kutathmini fursa za uwekezaji, umetembelea eneo linalopendekezwa kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda hicho lililopo Kata ya Ilolangulu, Wilaya ya Uyui. Eneo hilo linakadiriwa kuwa na zaidi ya ekari 2,000 na limependekezwa kutokana na nafasi yake ya kimkakati na upatikanaji wa ardhi ya kutosha kwa ajili ya shughuli za viwandani.
Baada ya kukagua eneo hilo leo, Desemba 5, 2025, wawakilishi wa United Capital Fertilizer wameeleza kuridhishwa kwao na mazingira ya eneo husika na hatua zilizochukuliwa na uongozi wa mkoa katika kuratibu mchakato wa uwekezaji.
Kwa mujibu wa tathmini za awali, uwekezaji huo unatarajiwa kuleta manufaa makubwa kwa wananchi wa Tabora na Tanzania kwa ujumla, ikiwemo kuongeza ajira kwa vijana, kuimarisha upatikanaji wa mbolea kwa bei nafuu, na kuchochea ukuaji wa kilimo cha kibiashara. Aidha, kiwanda hicho kitachangia kuongeza pato la mkoa na taifa kupitia kodi, pamoja na kuimarisha mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo ambao ni uti wa mgongo wa uchumi wa maeneo mengi nchini.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa