MKUU WA MKOA WA TABORA AONGOZA WANANCHI KUPIGA KURA, AIPONGEZA TUME HURU YA UCHAGUZI KWA MAANDALIZI MAZURI
Posted on: October 29th, 2025
Na. OMM Tabora.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Paulo Chacha, ameongoza wananchi wa mkoa huo katika kutimiza haki yao ya kikatiba kwa kujitokeza mapema kupiga kura na kuchagua viongozi wanaowataka, katika kituo cha kupigia kura cha Shule ya Msingi Kitete, leo asubuhi.
Baada ya kupiga kura, Mhe. Chacha alizungumza na waandishi wa habari na kuipongeza Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kwa maandalizi mazuri ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu, akibainisha kuwa zoezi linaendelea kwa amani, utulivu na ufanisi katika maeneo yote ya mkoa wa Tabora.
“Niwapongeze sana NEC kwa maandalizi bora na uendeshaji wa uchaguzi huu. Vituo vimefunguliwa kwa wakati, watendaji wanafanya kazi kwa weledi, na wananchi wanajitokeza kwa wingi kutekeleza wajibu wao wa kikatiba,” alisema Mhe. Chacha.
Aidha, amewataka wananchi wa Tabora kuendelea kudumisha amani na mshikamano wakati wote wa mchakato wa uchaguzi na kuhakikisha kila mmoja anatumia haki yake ya kidemokrasia kwa utulivu bila ushawishi au vurugu.
Zoezi la upigaji kura limeanza saa 1:00 asubuhi na linatarajiwa kufungwa saa 10:00 jioni katika vituo vyote nchini.