Na. Robert Magaka – Tabora.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Paulo Matiko Chacha, ameongoza hafla ya kuwaapisha wakuu wa wilaya wapya pamoja na viongozi wengine waandamizi, akiwataka kuzingatia maadili, weledi, na uadilifu katika utumishi wao kwa umma.
Katika tukio hilo lililofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Mtemi Isike Mwanakiyungi, walioapishwa rasmi ni Mhe. Upendo Bert Wella aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Tabora na Mhe. Thomas Mendraid Myinga, Mkuu mpya wa Wilaya ya Sikonge. Viongozi hao waliapishwa sambamba na wakurugenzi na makatibu tawala wapya wa wilaya, ambapo wote walikula kiapo cha uadilifu katika utumishi wa umma.
Viongozi wengine waliokula kiapo cha uadilifu mbele ya Mkuu wa Mkoa ni pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nzega, Ndg. Mwarami Seif, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua, Ndg. Shaban Kabelwa, Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Tabora, Dkt. Marco Pima, pamoja na Katibu Tawala wa Wilaya ya Kaliua, Ndg. Sosthenes Chakupanyuka.
Akizungumza kwa niaba ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora, Ndg. Said Juma Nkumba, aliwataka viongozi hao kufuata kwa karibu maelekezo ya serikali, kuwa na ushirikiano na watumishi waliowakuta, na kumtanguliza Mungu katika majukumu yao ya kila siku.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Dkt. John Mboya, aliwataka viongozi hao kutambua kuwa uteuzi wao ni heshima na imani kubwa waliyopewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Dkt. Mboya aliwataka kwenda kusimamia miradi ya maendeleo, kudhibiti matumizi ya fedha za umma kwa mujibu wa sheria za fedha na manunuzi ya umma, pamoja na kushughulikia miradi viporo. Alisisitiza umuhimu wa kusimamia mazingira na mapato ya halmashauri kwa uwazi na
Akihitimisha hafla hiyo,Mhe. Chacha aliwataka viongozi hao kutanguliza bidii na uadilifu katika kazi zao, hasa ikizingatiwa kuwa taifa linaelekea katika kipindi cha uchaguzi mkuu. Amesisitiza viongozi hao kuepuka kusimama katika upande wowote ule ambapo wagombea watafika katika maeneo yao kwa nia ya kutangaza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi.
Viongozi hao pia waliagizwa kuendeleza mambo mazuri yaliyoanzishwa na watangulizi wao na kuwa mstari wa mbele kulinda na kuimarisha amani, mshikamano, na maendeleo ya wananchi.
Kwa upande wao viongozi hao wameahidi kwenda kufanya kazi kwa bidii na kuwatumikia wananchi na kwamba watakwenda kuwa wasaidizi wazuri katika uongozi wa mkoa wa Tabora.
“Nakuadi tuliopishwa leo na wengine walioko hapa wote hatutakuangusha,tutafanya kazi kuwatumikia wananchi maana lengo kuu la serikali nikuleta ustawi kwa wananchi, tutakuwa wasidizi wazuri kwako wakati wote.” Alieleza Mhe. Myinga.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa