Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Mheshimiwa Sauda Mtondoo, amemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mheshimiwa Paul Chacha, katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani,Mei 1, 2025,yaliyofanyika kimkoa Uwanja wa Samora katika Halmashauri ya Mji wa Nzega.
Akisoma risala kwa niaba ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Mkoa wa Tabora (TUCTA), Mwalimu Silas John Mbuluma alieleza kuwa lengo la maadhimisho hayo ni kuwaleta pamoja wafanyakazi na waajiri ili kutathmini mafanikio ya mwaka uliopita, kujadili changamoto zilizopo, na kuweka mikakati ya kuboresha mazingira mahala pa kazi. Pia, alisema ni fursa ya kuhimiza nidhamu kazini na kuwakumbusha kuhusu sheria ya ajira na mahusiano kazini.
Mwalimu Mbuluma amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa ajira mpya katika sekta mbalimbali, hatua iliyowezesha kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi. Hata hivyo, walieleza changamoto zinazoikabili sekta ya umma, hasa katika kada ya elimu na afya, zikiwemo miundo ya utumishi isiyowahamasisha watumishi kujiendeleza kielimu, mishahara midogo isiyokidhi gharama za maisha, na kiwango kikubwa cha kodi (PAYE) kwenye mishahara yao.
Wafanyakazi pia waliitaka Serikali kufanyia kazi suala la leseni za kitaaluma zinazolipiwa kila mwaka na watumishi wa afya, wakipendekeza mzigo huo ubebwe na mwajiri. Aidha, walilalamikia utaratibu duni wa utoaji wa mikataba ya ajira, kunyimwa ruhusa, kutothibitishwa kazini, malimbikizo ya madeni, mapunjo ya mishahara, na huduma hafifu za bima ya afya licha ya makato kuendelea kufanyika kwa kiwango kilekile.
Akihutubia maelfu ya wafanyakazi na wananchi wa Nzega, Mheshimiwa Mtondoo alisema Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa wafanyakazi katika maendeleo ya taifa. "Haki na maslahi ya wafanyakazi ni jambo lisilopaswa kupuuzwa. Wafanyakazi ni uti wa mgongo wa taifa letu. Bila wao, hakuna maendeleo," alisisitiza.
Mheshimiwa Mtondoo aliwataka wafanyakazi kutumia busara kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kwa kuchagua viongozi waadilifu, wachapakazi na wanaojali maslahi ya wafanyakazi. Alihimiza ushiriki wa wafanyakazi katika mchakato wa uchaguzi kwa kujiandikisha na kuhakiki taarifa zao ili waweze kutumia haki yao ya kikatiba kuchagua viongozi sahihi. Pia aliwakumbusha kuwa, kwa mujibu wa sheria, wafanyakazi wana haki ya kugombea nafasi za uongozi.
Kuhusu suala la mishahara na marupurupu, Mheshimiwa Mtondoo alieleza kuwa Serikali inaendelea kujipanga ili kuboresha viwango vya mishahara na kuendeleza majadiliano na waajiri kupitia vyama vya wafanyakazi. Aidha, alisisitiza kuwa Serikali inapinga vikali aina yoyote ya unyonyaji na unyanyasaji kazini, na inaendelea kuwekeza katika mafunzo na ujuzi kwa wafanyakazi ili kuongeza tija katika utumishi wa umma.
Mhe. Mtondoo amemuelekeza Katibu Tawala wa mkoa kushughulikia kwa haraka changamoto zinazowezekana kutatuliwa katika ngazi ya mkoa, huku zile zilizo nje ya uwezo wake zikipelekwa kwenye mamlaka husika.
Akihitimisha hotuba yake, Mheshimiwa Mtondoo alitoa wito kwa wafanyakazi wote nchini kuzingatia haki na wajibu wao kwa uadilifu na weledi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni: "Uchaguzi Mkuu 2025, Utuletee Viongozi Wanaojali Haki na Maslahi ya Wafanyakazi – Sote Tushiriki."
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa