Na Mwandishi Wetu, Tabora.
Mkoa wa Tabora leo umehitimisha kwa mafanikio makubwa kambi ya michezo ya UMISSETA ngazi ya mkoa, ambapo Manispaa ya Tabora imeibuka kidedea kwa kushika nafasi ya kwanza kwa ujumla, ikiwa imejizolea alama 133. Hafla ya kufunga rasmi mashindano hayo ilifanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari ya wavulana Tabora, na kuhudhuriwa na maelfu ya wanamichezo, walimu, viongozi wa serikali na wazazi.
Akizungumza wakati wa kufunga mashindano hayo, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora ambaye pia ni Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia elimu, Mwalimu Upendo Rweyemamu, aliwapongeza wanamichezo wote kwa kushiriki kwa moyo wa uzalendo na ushindani wa kweli, akisema kuwa mashindano hayo yametimiza lengo la kuchagua wachezaji mahiri watakaoiwakilisha Tabora kwenye mashindano ya kitaifa ya UMITASHUMTA na UMISSETA yatakayofanyika mkoani Iringa kuanzia Juni 7 hadi Juni 30, 2025.
Katika matokeo ya jumla, Halmashauri ya Wilaya ya Igunga ilishika nafasi ya pili, ikifuatiwa na Kaliua katika nafasi ya tatu. Urambo ilichukua nafasi ya nne, Sikonge ya tano, Nzega Mji ya sita, Nzega ya saba, na Uyui ikifunga orodha ya washiriki kwa kushika nafasi ya nane.
Katika hatua ya kipekee na yenye hamasa, Mwalimu Upendo aliwakabidhi wanamichezo wa UMITASHUMTA bango maalum lenye ujumbe wa kuwahamasisha kutetea heshima ya Tabora kitaifa. Alisisitiza umuhimu wa maadili, nidhamu, na uzalendo miongoni mwa vijana hao, akibainisha kuwa michezo ni daraja la kukuza vipaji na kuimarisha mshikamano wa taifa.
Kauli mbiu ya mashindano ya Umitashumta na Umisseta mwaka huu ni: "Viongozi Bora ni Msingi wa Maendeleo ya Taaluma, Sanaa na Michezo – Shiriki Uchaguzi Mkuu 2025 kwa Amani na Utulivu." Kauli mbiu hii imekuwa mhimili wa hamasa kwa washiriki wote, ikielekeza fikra za vijana si tu katika ushindani wa kimchezo, bali pia katika kushiriki kwa tija kwenye masuala ya kijamii na kitaifa, hasa katika muktadha wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mapema mwezi Oktoba mwaka 2025.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa