Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Paulo Matiko Chacha, amefungua rasmi zoezi la huduma tembezi ya Samia, inayojishughulisha na utatuzi wa changamoto za walimu nchini, katika ukumbi wa mikutano wa Isike Mwanakiyungi, mkoani Tabora.
Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Bi. Leah Ulaya, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kukiamini Chama cha Walimu Tanzania kuhusika na zoezi hili muhimu la kitaifa, linalolenga kuhakikisha changamoto zote za walimu zinatatuliwa kwa wakati, na kwamba kila mwalimu anafanya kazi katika ufanisi na akiwa katika hali bora.
Bi. Ulaya aliyasema hayo wakati akitoa salamu za CWT mbele ya walimu kutoka wilaya za mkoa wa Tabora pamoja na mikoa jirani waliohudhuria kwa ajili ya kutatuliwa changamoto zao.
Akiongea na walimu wa mkoa wa Tabora, Mhe. Paulo Chacha amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake na kuelekeza jambo hili lifanyike mikoa yote ya Tanzania, na ana matumaini kwamba sasa changamoto nyingi za walimu zitapatiwa ufumbuzi. Aidha, amewaasa walimu nchini kushikamana kwani umoja ni nguvu ya kufanikisha jambo lolote katika jamii.
“Tulitegemea mtengeneze jumuiya yenye nguvu badala ya kufanya mchezo wa kumeguka. Umoja siku zote ni nguvu. Ni bora kupambana ndani ya chama kuondoa tofauti zenu kuliko kumeguka na kuunda utitiri wa vyama visivyo na msaada kwa wanachama wake,” alisema Mhe. Chacha.
Kwa upande wao walimu wa mkoa wa Tabora wamefarajika na ujio wa huduma hii tembezi na wanamatumaini makubwa sasa kuwa kero zao nyingi zitakwenda kutatuliwa, ikiwa ni pamoja na mapunjo ya mishahara,madeni ya fedha za uhamisho pamoja na changamoto zingine za kiutumishi.
Kliniki hii tembezi ya msaada wa Samia (Samia Teachers Mobile Clinic) inaratibiwa na Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Utumishi, Ofisi ya Rais, Tamisemi, Wizara ya Elimu pamoja na Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), ikiwa mkoa wa Tabora ni wa 15 kufikiwa na huduma hii nchini.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa