Na Mwandishi Wetu – Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Tabora.
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi, amefanya ziara mkoani Tabora kukagua hali ya mawasiliano katika wilaya za Uyui na Tabora Manispaa. Ziara hiyo imelenga kujiridhisha na upatikanaji wa huduma za mawasiliano, pamoja na kuhimiza wananchi kutunza miundombinu ya mawasiliano kwa manufaa ya maendeleo yao.
Akiwasilisha taarifa ya hali ya mawasiliano katika mkoa wa Tabora, Meneja wa TCRA Kanda ya Kati, Mhandisi Asajile John, alisema kuwa TCRA inaendelea kusimamia usambazaji wa huduma za mawasiliano kwa kuzingatia jiografia na idadi ya watu. Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 98 ya wananchi wa Tabora wanapata mawasiliano ya 2G, asilimia 81.6 wanapata 3G, asilimia 72.1 wanatumia 4G, huku asilimia 3.2 wakifikiwa na mtandao wa 5G. Aidha, kwa ujumla asilimia 91 ya Watanzania wanapata huduma za 3G, hatua inayowezesha wananchi kuingia katika uchumi wa kidijiti. Kufikia Desemba 2024, Tabora ilikuwa na laini za simu milioni 4.28, idadi inayozidi wakazi wa mkoa huo kwa asilimia 123.8 kulingana na sensa ya mwaka 2022.
Katika hatua nyingine, vitendo vya uhalifu mtandaoni vimepungua kwa asilimia 79.3 mwaka 2024 ikilinganishwa na 2023, ambapo kulikuwa na rekodi ya majaribio 590 ya uhalifu mtandaoni. Mafanikio haya yanatokana na juhudi za serikali kutoa elimu kwa umma kuhusu usalama mtandaoni.
Mhe. Mahundi alitembelea ujenzi wa minara ya mawasiliano inayojengwa kwa ushirikiano wa sekta binafsi na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF). Mnara wa mtandao wa Yas unaojengwa kwa gharama ya shilingi milioni 290 katika kata ya Ifucha, Manispaa ya Tabora, pamoja na mnara wa Halotel unaojengwa katika kijiji cha Mwakashindye, kata ya Ibiri, wilayani Uyui, ni miongoni mwa juhudi za kuimarisha mawasiliano nchini.
Katika hotuba yake, Mhe. Mahundi aliwataka wananchi kuitunza miundombinu hiyo na kuzingatia matumizi sahihi ya teknolojia kwa maendeleo yao, huku akiwatahadharisha wananchi kuepuka kuwa sehemu ya watu wanaoihujumu serikali kwa kuharibu miundombinu hiyo.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote Kanda ya Kati, Ndg. Shirikisho Mpunji, alisema kuwa serikali imeendelea kujenga minara ya mawasiliano katika maeneo yenye changamoto. Hadi sasa, minara 118 yenye thamani ya shilingi bilioni 19 imekamilika katika kata 86 za Tabora, huku awamu ya tisa ya ujenzi wa minara mingine ikitarajiwa kutangazwa hivi karibuni.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Tabora Kaskazini, Mbunge wa jimbo hilo, Mhe. Almasi Maige, aliishukuru serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kupeleka zaidi ya shilingi bilioni 2.2 kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika sekta za afya, elimu na miundombinu, hatua inayowanufaisha wakazi wa wilaya ya Uyui kwa kiasi kikubwa.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa