Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Dkt. John Mboya, ameongoza kikao kazi cha kujadili utekelezaji wa shughuli za kilimo kwa kuzingatia utabiri wa hali ya hewa uliotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa msimu huu wa kilimo.
Kikao hicho, kilichowakutanisha maafisa kilimo kutoka halmashauri zote za Mkoa wa Tabora na wataalamu kutoka Ofisi ya Kilimo ya Mkoa, kililenga kuweka mikakati ya kuongeza tija ya uzalishaji huku wakulima wakihimizwa kulima mazao yanayostahimili ukame kutokana na mwenendo wa mvua unaotarajiwa kuwa wa wastani hadi chini ya wastani. Akizungumza wakati wa kufungua kikao hicho, Dkt. Mboya aliwataka wataalamu wa kilimo kuhakikisha wanakuwa karibu na wananchi, kuwashauri kwa wakati, na kusimamia ipasavyo shughuli za uzalishaji.
“Kuweni karibu na wananchi ili muweze kuwashauri vema wakulima wetu. Natoa wito kwa sekta binafsi na sekta za umma kutekeleza wajibu wao kwa kuzingatia taarifa za utabiri wa hali ya hewa, ili wananchi waweze kufanya maamuzi sahihi kwa ujasiri,” alisema Dkt. Mboya.
Kwa upande wake, Meneja wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Kanda ya Magharibi – Tabora, Waziri Omari Waziri, aliwasilisha taarifa ya utabiri wa msimu akibainisha kuwa mvua za msimu huu zinatarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani katika maeneo mengi ya Mkoa wa Tabora.
“Wananchi wanapaswa kuzingatia ushauri wa wataalamu wa kilimo na mifugo ili waweze kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na mwenendo wa mvua,” alifafanua Waziri.
Aliongeza kuwa TMA inasisitiza wadau wote wa sekta mbalimbali kama wafugaji, mamlaka za maji, afya na wanyamapori kuendelea kutumia taarifa za hali ya hewa katika kupanga shughuli zao za kila siku.
Naye Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia Kilimo, Mifugo, Uzalishaji na Ushirika, Abaraham Mndeme, alieleza kuwa kutokana na utabiri huo, halmashauri zote zimeelekezwa kuwahimiza wakulima kulima mazao yanayostahimili ukame kama vile mtama, uwele na mihogo.
“Wakurugenzi wa halmashauri wahakikishe wanawafikia wananchi na kuwaelimisha kuhusu umuhimu wa kufuata ushauri wa wataalamu ili kuepuka hasara katika uzalishaji,” alisema Mndeme.
Kikao hicho kilihitimishwa kwa majadiliano ya mipango na mikakati ya utekelezaji wa shughuli za kilimo kulingana na hali ya hewa, ambapo kila halmashauri ilitakiwa kuandaa mpango wa kuelimisha wakulima na wafugaji kuhusu mbinu bora za kilimo na ufugaji endelevu.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa