Waziri wa Afya, Mhe. Jenista Joackim Mhagama, ameongoza uzinduzi wa mpango maalum wa huduma za kibingwa kutoka kwa madaktari bingwa wa "Mama Samia Awamu ya Tano" katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Isike Mwanakiyungi. Mpango huu unaolenga kuwafikia wananchi walioko mbali na hospitali kubwa, umetajwa kuwa ishara ya ubunifu, uzalendo na upendo kwa taifa.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mhe. Deusdedith Katwale alitoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wizara ya Afya kwa kuleta huduma hizi muhimu. Alieleza kuwa mpango huu umesaidia wananchi wasiokuwa na uwezo wa kufuata huduma za kibingwa katika hospitali kubwa, hivyo kuokoa maisha na kuboresha afya za jamii za pembezoni.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Dkt. John Mboya, alieleza kuwa mkoa umehamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kupata huduma hizo, akimshukuru Waziri Mhagama kwa kuleta madaktari bingwa mkoani humo. Alisisitiza kuwa ushirikiano baina ya viongozi na wataalamu wa afya utaongeza ufanisi wa huduma hizi.
Katika hotuba yake, Waziri Mhagama aliwapongeza madaktari bingwa kwa juhudi kubwa wanazozifanya nchi nzima, akibainisha kuwa mpango huu ni kipaumbele cha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya mwaka 2024, zaidi ya wananchi 154,015 walihudumiwa na madaktari bingwa waliotembelea halmashauri zote 184 za Tanzania Bara.
Aidha, Waziri alisifu mafanikio ya sekta ya afya katika kupunguza vifo vya akina mama wajawazito kwa asilimia 80, mafanikio yaliyowezesha Tanzania kupata tuzo ya kimataifa ya "Goalkeepers" kutoka Taasisi ya Gates. Alitoa wito kwa madaktari kuendeleza maadili ya utabibu, kuelimisha wenzao na kuhudumia wananchi kwa moyo wa uzalendo.
Uzinduzi huo pia ulihudhuriwa na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini Tanzania, Dkt. Charles Sagoe-Moses, ambaye alipongeza jitihada za serikali za kufikisha huduma bora za afya katika maeneo yenye changamoto za miundombinu, akisisitiza umuhimu wa kuendeleza juhudi hizi kwa ustawi wa wananchi.
MWISHO.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa