Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amefanya ziara ya kukagua miradi ya maendeleo wilaya ya Igunga katika jimbo la Igunga na Manonga mkoani Tabora.
Miradi aliyokagua,kuzindua na kuweka mawe ya msingi katika wilaya ya Igunga ni pamoja na mradi wa upanuzi wa mtandao wa kusambaza maji safi na salama ya ziwa Victoria kutoka makomero mpaka Mgongoro katika kijiji cha Mwamayoka wenye thamani ya shilingi milioni 840.7 mradi huu utakwenda kukamilisha usambazaji wa maji safi na salama kwa wilaya ya Igunga kwa asilimia 100 pindi miundombinu ya ugawaji maji katika Kijiji cha Mwamayoka na vitongoji vyake kukamilika.
Vilevile amekagua na kuweka mawe ya msingi katika mradi wa vibanda vya biashara,ujenzi wa shule ya sekondari Seif Gulamali pamoja na mradi wa usambazaji wa maji kutoka Ziba hadi Nkinga awamu ya pili wenye gharama ya shilingi bilioni 2.49.
Akitoa taarifa ya maendeleo ya mkoa, Kaimu Mkuu wa mkoa wa Tabora Mhe. Cornel Lucas Magembe amesema serikali ya awamu ya sita kwa sekta ya afya pekee imekwisha toa fedha za miradi ya maendeleo kwa ajili ya ujenzi wa hospitali za wilaya,vituo vya afya pamoja na zahanati shilingi bilioni 30.2 na shilingi bilioni 132 kwa ajili ya sekta ya elimu ikihusisha ujenzi wa shule za sekondari 25,shule za msingi 22,mabweni 90 pamoja na nyumba 16 za walimu.Miradi hii imesaidia kuboresha utoaji wa huduma za afya na elimu kwa kiwango kikubwa sana, hivyo hana budi kuishukuru na kuipongeza serikali kwa jitihada kubwa za kuwaletea wananchi maendeleo.
Kwa upande wao waheshimiwa wabunge wa wilaya ya Igunga, Mhe. Nicholaus Ngassa pamoja na Mhe. Seif Gulamali wameipongeza serikali ya awamu ya sita kwa kutoa fedha nyingi za miradi ya maendeleo mkoani Tabora hususan wilaya ya Igunga na kuleta matokeo makubwa katika kutatua kero za maji, na sasa kero ya maji inakwenda kuwa historia katika wilaya ya Igunga.
Akiongea na wananchi wa wilaya ya Igunga kwa nyakati tofauti Mhe. Majaliwa amefurahishwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika wilaya ya Igunga ambapo thamani ya fedha inaonekana wazi kwa jinsi miradi hiyo ilivyotekelezwa kwa viwango vizuri.Ameagiza uongozi wa wilaya ya Igunga kuhakikisha inatenga fedha kwa ajili ya uchimbaji wa mabwawa (mabakuli) ya kunyweshea mifugo kwa ajili ya kusaidia shughuli za wafugaji yatakayoungwanishwa na mtandao wa maji yaliyozinduliwa pamoja na kutenga fedha za mapato ya ndani shilingi milioni 50 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati katika kijiji cha Mwamayoka wasisubiri fedha kutoka serikali kuu, kwani ujenzi wa zahanati hiyo inayohitajiwa na wananchi haraka ipo ndani ya uwezo wa halmashauri kupitia fedha za mapato ya ndani.
Mhe. Majaliwa amewahakikishia wananchi wa mkoa wa Tabora kuwa serikali ipo kazini kuendelea kuwahudumia wananchi kwa ufanisi mkubwa,wao waendelee kuchapa kazi kwa bidii hii ni nchi yao na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan yupo kazini kuhakikisha kuwa wanapata maendeleo makubwa katika nyanja mbalimbali za kiuchumi.
Vilevile Mhe. Majaliwa ametoa maelekezo ya serikali ikiwa ni pamoja na kusisitiza matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wananchi wa wilaya ya Igunga kwani gharama za nishati mbadala kama vile umeme na gesi ni nafuu sana na unatuza mazingira na kurahisisha shughuli za kiuchumi.
Ametoa rai pia kwa wananchi kupeleka watoto shule,kwani elimu ni bure na serikali ipo makini kuhakikisha michango isiyo na tija shuleni inakomeshwa sambamba na kumlinda mtoto wa kike na wakiume ili wafikie malengo katika safari yao ya kielimu.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anatarajia kuhitimisha ziara yake mkoani Tabora hapo kesho kwa kukagua miradi ya maendeleo katika wilaya ya Nzega pamoja na kuzungumza na wananchi.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa