UTANGULIZI
-
Wilaya ya Urambo ni kati ya Wilaya 7 zinazounda Mkoa wa Tabora. Wilaya hii ilianzishwa tarehe 19/07/1975, ina tarafa 2 ( Ussoke na Urambo ) ina ukubwa wa eneo lenye km2 6,110 sawa na 8% ya eneo la Mkoa, Makao makuu ya Wilaya yapo katika mji mdogo wa Urambo umbali wa km 90 kutoka Tabora Mjini.
-
Wilaya hii imepakana na Wilaya ya Sikonge na Uyui kwa upande wa Mashariki, na inapakana na Wilaya ya Mpanda (Mkoa wa Katavi) kwa upande wa Kusini, kwa upande wa Kaskazini Magharibi inapakana na Wilaya ya Kaliua.
IDADI YA WATU.
-
Kulingana na sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, Wilaya ya Urambo ina jumla ya wakazi wapato 192,781. Kati yao Wanaume 95,997 sawa na 49.80% na Wanawake 96,784 sawa na 50.2% . Wilaya ina jumla ya kaya 32,675 kwa wastani wa ukubwa wa kaya moja ni watu 5.9 ongezeko la watu kwa mwaka inakisiwa kuwa 4.8%.
HALI YA UCHUMI NA MAENDELEO YA WILAYA.
-
Uchumi wa Wilaya unategemea zaidi kilimo ambacho kinaajiri takribani asilimia 80 ya wakazi wote wa Wilaya hii. Mapato yanayotokana na ufugaji, Uvuvi, Ufugaji wa nyuki na shughuli za viwanda vidogo vidogo ni ajira mbadala zinazochangia katika pato la wakazi wetu.
-
Pato la Wilaya ya Urambo katika mwaka 2012/2013 hadi Desemba, 2012 lilikuwa Tshs. 77,822,778,064/= ikilinganishwa na idadi ya watu 192,781 na hivyo pato la mtu ni sawa na Tshs. 403,685/=. Aidha wastani wa pato la mtu kwa mwaka liliongezeka kutoka Tshs. 172,000/= mwaka 2002 hadi Tshs. 403,685/= mwaka 2012, sawa na ongezeko la Tshs. 231,685/=.
HALI YA ULINZI NA USALAMA
-
Hali ya ulinzi na usalama katika Wilaya yetu kwa ujumla ni nzuri; na hii inachangiwa na uwepo wa ulinzi shirikishi kupitia Polisi jamii. Mpango huu muhimu ni wa kudumu kwa kushirikisha jeshi la mgambo katika suala la ulinzi kwa kuwatambua, kuwajali na kuwathamini.
-
Hata hivyo wilaya inaendelea kukabiliana na matukio mara kwa mara ya makosa ya jinai yakiwemo ya unyang’anyi wa kutumia silaha na nguvu, Uvunjaji, Wizi wa pikipiki,Wizi wa mifugo,kuchoma nyumba moto n.k. Mauaji yanayotokea katika Wilaya hii mara nyingi yanatokana na kulipiza kisasi, imani za kishirikina na matukio machache ya kugombea mali.
-
Kufuatia hali hiyo wilaya inashirikiana na Wilaya jirani katika mkakati wa kuimarisha Ulinzi na usalama na kubadilishana taarifa za kiuharifu miongoni mwetu na Wilaya zinazotuzunguka.
HALI YA UTOAJI HUDUMA KISEKTA
-
Shughuli ambazo zimekuwa zikitekelezwa na Wilaya kisekta katika utoaji wa huduma za kijamii na kiuchumi kama ifuatavyo:-
SEKTA YA UTAWALA NA UTUMISHI.
-
Wilaya ina jumla ya watumishi 1,458 kutoka katika kada mbalimbali za utumishi kama zifuatavyo:- Utawala na Utumishi 100, Elimu Sekondari 209,Elimu Msingi 835 , Afya 215, Kilimo Umwagiliaji na Ushirika 15,Mifugo na Uvuvi 9,Ardhi na Maliasili 6, Maji 7, Ujenzi 18, Watendaji wa Vijiji 43 na Usafi na Mazingira 1.
-
CHANGAMOTO
-
Watumishi walioajiriwa kuomba kuhama kufuata wenzi wao baada ya kukaa muda
-
Ufinyu wa bajeti
-
Utoro kazini
-
Watumishi wapya Kushindwa kuripoti na Serikali kutoleta watumishi kulingana na ikama iliyoidhinishwa.