Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, chini ya uongozi wa Mwenyekiti wake, Mhe. Deodatus Philip Mwanyika, Mbunge wa Njombe Mjini imetembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa jengo la Bodi ya Tumbaku Kanda ya Magharibi, unaojengwa katika mkoa wa Tabora kwa gharama ya shilingi bilioni 1.23.
Mhe. Mwanyika ameipongeza Bodi ya Tumbaku kwa kuanzisha mradi huu muhimu, ambao utasaidia katika usimamizi wa zao la tumbaku na kutoa mchango mkubwa katika mapato ya serikali kupitia upangishaji wa sehemu ya jengo hilo kwa matumizi ya kibiashara.
Wajumbe wa kamati hiyo, licha ya kubaini kasoro chache katika utekelezaji wa mradi huo, walionesha kuridhika na ubora wa kazi inayofanywa hadi sasa. Walitoa maelekezo kwa Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Tumbaku, Ndg. Stanley Mnozya, kuhakikisha kwamba changamoto zilizojitokeza zinatatuliwa kwa haraka na kwa ufanisi.
Akihitimisha kikao cha majumuisho, Mhe. Mwanyika alisisitiza umuhimu wa usimamizi makini na wa kitaalamu katika kazi za ujenzi wa miradi ya umma, kuanzia hatua za awali hadi mwisho. Aliipongeza Bodi ya Tumbaku kwa mabadiliko ya kimkakati yaliyofanywa kwenye mradi huo, ambapo jengo hilo litakuwa kitega uchumi, jambo litakalosaidia kuongeza faida kwa taasisi hiyo.
Aidha, Mhe. Mwanyika alitoa maelekezo kwa mkandarasi wa mradi huo, Suma JKT, kuhakikisha kuwa anakamilisha kazi kwa weledi na ubora wa hali ya juu, na kwamba mradi huo ukamilike kwa wakati.
Kwa upande wake, Ndg. Victor Mwambalaswa, Mwenyekiti wa Bodi ya Tumbaku Tanzania, kwa niaba ya bodi hiyo, aliishukuru Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo kwa kutembelea mradi huo na kutoa maelekezo ya muhimu ya kisekta. Ameihakikishia kuwa maelekezo yote yaliyotolewa yatazingatiwa na kufanyiwa kazi ili kuboresha utekelezaji wa mradi kwa ufanisi.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa