Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Mhe. Upendo Wella, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, ameongoza watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora katika sherehe ya kuukaribisha Mwaka Mpya 2026 pamoja na kuwaaga watumishi waliokamilisha utumishi wao wa umma kwa mujibu wa sheria. Sherehe hizo zimefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya JM Mjini Tabora.
Akitoa nasaha zake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora,Dkt. John Mboya, amemshukuru Mwenyezi Mungu kwa mafanikio ya utekelezaji wa majukumu kwa mwaka uliopita na kuwasisitiza watumishi kuongeza bidii, upendo na mshikamano kazini. Ameeleza kuwa umoja na ushirikiano ni msingi wa kutekeleza kwa ufanisi maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ya kuwahudumia wananchi kwa uadilifu na kuhakikisha wanapata tabasamu.
Kwa upande wake, mgeni rasmi Mhe. Wella, akitoa salamu za Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paulo Chacha, amewahimiza watumishi kufanya kazi kwa bidii na weledi, akisisitiza kuwa dhamana waliyopewa ni kielelezo cha imani ya Rais kwa viongozi na watumishi wa umma.
Katika sherehe hizo, wastaafu wamepongezwa kwa kumaliza salama safari ya utumishi wa umma na kushukuriwa kwa mchango wao kwa Serikali. Wastaafu hao, kwa pamoja, wamewashauri watumishi wanaoendelea kujiandaa mapema kwa maisha ya kustaafu. Watumishi walioagwa ni pamoja na Simon Mality, Mhasibu Mkuu wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mussa Mussa, Afisa Mifugo, pamoja na Pastory Mashiku aliyehamia Wilaya ya Rorya mkoani Mara. Aidha, sherehe zimeambatana na mapokezi ya watumishi waliohamia ofisi ya Mkuu wa mkoa akiwemo Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu Bi. Upendo Joseph Haule na Masunga Maduhu,Katibu Muhtasi.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa