Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Paulo Matiko Chacha, amefanya ziara ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi katika Wilaya ya Tabora na Nzega. Katika ziara hiyo, Mhe. Chacha alikutana na watumishi wa Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA) pamoja na wale wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).
Katika hatua muhimu, Mhe. Chacha alimsimamisha kazi Meneja wa GPSA Mkoa wa Tabora, Bw. Mayala Mbuli, ili kupisha uchunguzi zaidi kuhusu tuhuma zinazomkabili za utovu wa nidhamu na kushindwa kutoa huduma bora kwa wateja. Aidha, alimuagiza Meneja wa TANROADS Mkoa wa Tabora, Mhandisi Raphael Mlimaji, kuchukua hatua dhidi ya watumishi wawili wa TANROADS kwa tuhuma za kupokea rushwa katika mzani mdogo wa Tuli.
Ziara ya Mhe. Chacha ilikamilika wilayani Nzega, ambapo alitembelea machimbo ya dhahabu katika Kijiji cha Isanga, Kata ya Lusu. Akiwa huko, aliwashauri wananchi kuwa makini na matapeli wanaotumia hadaa kuwadanganya viongozi wa serikali na wananchi kwa manufaa yao binafsi. Mhe. Chacha alimpongeza Bi. Rehema Salim, Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji wa Dhahabu cha Mkombozi, kwa ujasiri wake wa kutoa taarifa kuhusu matapeli waliovamia eneo la wachimbaji na kuanza kuchimba dhahabu kinyume cha sheria.
Vilevile, Mhe. Chacha alimuamuru Mkuu wa Chuo cha Madini Tawi la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bw. Abrahamu Lwakajunguti, kuondoka mara moja katika eneo hilo kwa tuhuma za kuruhusu wachimbaji kuingia katika eneo la chuo hicho na kuchimba dhahabu kinyume cha sheria. Pamoja na kuonesha utovu wa nidhamu kwa viongozi pamoja na wananchi wa eneo hilo.
Ziara ya Mhe. Chacha ilihitimishwa kwa agizo la kumaliza mgogoro kati ya Kampuni ya Uchimbaji wa Madini ya Savanna Reef na mchimbaji mdogo wa madini, Bw. Nshishi. Alisisitiza kuwa mgogoro huo hauwezi kufaidisha pande yoyote na unadumaza tu shughuli za uzalishaji katika eneo hilo, hivyo alitoa agizo la kumaliza tofauti hizo haraka.
Ziara hii inadhihirisha juhudi za Mhe. Chacha katika kutatua changamoto za wananchi na kuhamasisha uwajibikaji katika taasisi za umma na sekta ya uchimbaji madini.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa