Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, amefanya ziara mkoani Tabora kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi wa wilaya ya Igunga
Moja ya miradi aliyoikagua Dkt. Gwajima ni ujenzi wa vyumba 4 vya madarasa na matundu 6 ya vyoo katika shule ya msingi Nyandekwa, wilayani Igunga. Mradi huo una thamani ya shilingi milioni 117 na unatarajiwa kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa watoto, hivyo kuongeza ufanisi wa kielimu katika shule hiyo.
Pia, Dkt. Gwajima amezindua matumizi ya mashine ya kulimia kwa kikundi cha wanawake cha Mwendokasi, kilichojikita katika kilimo cha mpunga katika kata ya Igunga, Kitongoji cha Mwanzugi. Mradi huu unafadhiliwa na mkopo usio na riba wa shilingi milioni 30 kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Igunga na utawafaidi wanawake hao katika kuboresha uzalishaji bora wa zao la mpunga.
Akiongea na wananchi wa Mwanzugi, Dkt. Gwajima ametoa wito kwa jamii kuchukua hatua madhubuti kukabiliana na vitendo viovu, hasa dhidi ya watoto. Amesisitiza umuhimu wa wazazi na walezi kusimamia maadili katika familia zao ili kuwaepusha watoto na vitendo viovu, kama vile ubakaji, ulawiti, na matumizi ya dawa za kulevya. Dkt. Gwajima amekumbusha kuwa mmomonyoko wa maadili umekithiri na wazazi wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuzungumza na watoto wao kuhusu umuhimu wa maadili mema katika jamii.
Aidha, Waziri Gwajima ametoa wito kwa jamii kubadilisha mtazamo wao kuhusu upatikanaji wa taarifa za maendeleo. Akiwataka wananchi kuhamasika na kuchukua hatua za haraka kutafuta taarifa za maendeleo kama wanavyofanya katika masuala mengine ya burudani, kama vile michezo ya mpira. Amesema kuwa hii itasaidia kupunguza malalamiko na kuongeza uelewa kuhusu miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali.
Dkt. Gwajima ameongeza kuwa serikali ya Tanzania imetoa zaidi ya shilingi trilioni 1.1 kwa ajili ya miradi ya maendeleo mkoani Tabora pekee.Jambo ambalo ni muhimu kwa maendeleo ya watu lakini bado wananchi wengi hawana taarifa juu ya mambo mazuri kama haya yanayotekelezwa na serikali ya awamu ya sita.
Ziara ya Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima inaendelea mkoani Tabora kwa lengo la kuhamasisha wananchi kuchangia katika maendeleo ya taifa na kuimarisha ushirikiano baina ya serikali na wananchi katika kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi.
Top of Form
Bottom of Form
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa