Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Paul Matiko Chacha, amefungua kikao kazi cha maafisa elimu kata na wakuu wa shule za sekondari mkoa wa Tabora kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa mkoa wa Tabora, Isike Mwanakiyungi. Kikao hicho ni cha siku mbili, na lengo lake kuu ni kuwajengea uwezo walimu wakuu pamoja na maafisa elimu kata ili kuboresha taaluma mkoani Tabora.
Katika ufunguzi wa kikao hicho, Katibu Tawala Msaidizi Elimu, Bi. Upendo Rweyemamu, ameipongeza na kuishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya elimu, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa shule za msingi na sekondari katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Tabora. Amesema kuwa juhudi hizi zimeleta mabadiliko chanya katika mazingira ya utoaji elimu, na kwamba wanafunzi sasa wanapata mazingira bora zaidi ya kujifunza.
Hata hivyo, Bi. Rweyemamu amekiri uwepo wa changamoto zinazoukabili mkoa katika sekta ya elimu. Amebainisha kuwa utoro na mdondoko wa wanafunzi ni miongoni mwa sababu kubwa zinazozorotesha maendeleo ya elimu na ufaulu mkoani Tabora pamoja ushirikiano hafifu kutoka kwa wazazi, hasa katika suala la kuchangia chakula shuleni, umeendelea kuwa kikwazo kikubwa katika kuboresha mazingira ya kujifunza.
Katika hatua nyingine, Mhe. Paul Chacha ametoa pongezi kwa walimu kwa juhudi zao katika kudhibiti vitendo viovu, ikiwemo ukatishaji wa elimu kwa watoto wa kike, vitendo ambavyo vinavunja maadili ya jamii. Amesisitiza kwamba walimu wanajukumu la kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha watoto wote wanapata elimu bila vikwazo vya kijinsia au kijamii.
Akizungumzia changamoto ya utoro na mdondoko, Mhe. Chacha ametoa agizo kwa kila mzazi mwenye mtoto wa umri wa kwenda shule ahakikishe anahudhuria shule mara tu zitakapofunguliwa. Amesema kuwa atakayeshindwa kutekeleza wajibu huo atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Aidha, Mhe. Chacha amewasihi walimu kudumisha umoja na mshikamano katika kazi zao, akisisitiza kuwa umoja ndio nguzo ya mafanikio. Ametoa wito kwa walimu kutojiingiza katika migawanyiko ya ndani na kuwa na kauli moja katika kutatua changamoto zinazojitokeza. "Msifikiri ni sifa kutengana, jitahidini sana muwe na kauli moja, chagueni wawakilishi wenye kuwaunganisha na wala msikubali kushusha thamani yenu kwa vitu vidogo, Walimu hamuwezi kuwa na sauti moja yenye nguvu mkiwa mmemeguka vipande vipande.”amesisitiza.
Kikao kazi hiki kinatarajiwa kutoa ufumbuzi wa haraka kwa changamoto mbalimbali zinazoukabili mkoa katika sekta ya elimu na kujenga uwezo kwa walimu na maafisa elimu kata katika kuhakikisha maendeleo ya elimu yanafikiwa kwa haraka.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa