Washiriki wa Kozi ya 14 kutoka Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC), wakitoka katika mataifa saba ambayo ni Misri, Malawi, Rwanda, Burundi, Kenya, India na Tanzania, wamewasili mkoani Tabora kwa ziara ya mafunzo kwa vitendo itakayodumu kwa muda wa siku sita, ikiwa na lengo la kujifunza na kujionea utekelezaji wa shughuli mbalimbali katika nyanja za siasa, uchumi na maendeleo ya kijamii.
Ziara hiyo mkoani Tabora inaongozwa na Kaimu Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi, Brigedia Jenerali Charles Ndiege, ambapo wamepokelewa rasmi na Mkuu wa Wilaya ya Kaliua, Mhe. Dkt. Gelard Mongella, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora.
Katika kipindi cha ziara yao, washiriki wa mafunzo hayo wanatarajia kutembelea na kujionea miradi na taasisi mbalimbali za kimkakati ikiwemo Kiwanda cha kutengeneza mkaa mbadala cha Kuja na Kushoka kilichopo Manispaa ya Tabora, Ranchi ya kisasa ya ng’ombe wa maziwa wilayani Uyui, pamoja na mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi katika eneo la Sojo.
Aidha, kundi hilo pia linatarajia kutembelea Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) – Tumbi, pamoja na Kiwanda cha kuchakata mazao ya nyuki kilichopo wilayani Sikonge, ili kupata uelewa wa moja kwa moja kuhusu jitihada za Serikali katika kuimarisha uzalishaji na kukuza uchumi wa viwanda.
Ziara hiyo ni sehemu ya mafunzo ya vitendo kwa washiriki wa Kozi ya 14 ya Chuo cha Taifa cha Ulinzi, yenye lengo la kuwajengea uelewa wa kina kuhusu uhalisia wa utekelezaji wa sera na mipango ya maendeleo ya Serikali katika mikoa ya Mwanza, Geita, Singida, Kilimanjaro, Tanga, Njombe, Iringa na Tabora.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa