Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Wakili Ng’wasi Kamani, amefanya ziara ya kikazi mkoani Tabora akitembelea wilaya za Nzega na Igunga kwa lengo la kukagua utekelezaji wa shughuli za sekta ya mifugo na kusikiliza kero pamoja na changamoto zinazowakabili wafugaji ili kuboresha ustawi wa sekta hiyo.
Akiwa wilayani Nzega, Mhe. Kamani alitembelea mnada wa mifugo uliopo Kata ya Ndala, ambako alikutana na wafugaji na kufanya mazungumzo ya ana kwa ana. Wafugaji waliwasilisha changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa mbegu bora za mifugo, uhaba wa maeneo ya malisho, miundombinu duni ya barabara katika eneo la mnada, ugumu wa kupata mikopo pamoja na kukosekana kwa uzio wa kuimarisha usalama wa mnada.
Akizungumza na wafugaji hao, Mhe. Kamani aliwasisitiza kuzingatia taratibu na kanuni za uendeshaji wa masoko ya mifugo, akieleza kuwa taratibu hizo zimewekwa kwa lengo la kuhakikisha uwazi, usimamizi mzuri na ufuatiliaji wa biashara ya mifugo ili kuwalinda wafugaji na wanunuzi kwa ujumla.
Akijibu changamoto zilizowasilishwa, Naibu Waziri alisema Serikali tayari imechukua hatua za makusudi za kuzalisha na kusambaza mbegu bora za mifugo ili kuongeza tija, kuboresha uzalishaji na kuinua uchumi wa wafugaji kupitia upatikanaji wa mifugo bora yenye thamani ya kibiashara.
Akihitimisha ziara yake, Mhe. Kamani aliwaelekeza wataalam wa sekta ya mifugo kuacha kufanya kazi kwa kusubiri wateja ofisini na badala yake kushuka uwandani kuwafuata wafugaji katika maeneo yao. Alisisitiza umuhimu wa kutoa elimu ya ufugaji bora, matumizi ya mbegu bora za mifugo na malisho, pamoja na kuhamasisha utekelezaji wa maboresho yanayoendelea kufanywa na Serikali katika sekta ya mifugo.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa