Washiriki kutoka Chuo cha Taifa cha Ulinzi - Tanzania (NDC) wamehitimisha rasmi ziara yao ya kikazi mkoani Tabora kwa kutembelea kiwanda cha kati cha kuchakata mazao ya nyuki kilichopo wilayani Sikonge, ikiwa ni sehemu ya ratiba ya mafunzo yao ya vitendo yenye lengo la kuoanisha nadharia na uhalisia wa utekelezaji wa sera na mipango ya maendeleo ya Serikali.
Timu hiyo ya washiriki wa Kozi ya 14 ilipokelewa wilayani Sikonge na Mkuu wa Wilaya, Mhe. Thomas Myinga, katika ofisi yake, ambapo walipata fursa ya kujitambulisha kabla ya kuelekea katika kiwanda hicho cha kuchakata mazao ya nyuki kwa ajili ya kujionea shughuli za uzalishaji na thamani-nyongeza katika sekta ya ufugaji nyuki.
Akizungumza kwa niaba ya washiriki hao, Kaimu Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi, Brigedia Jenerali Charles Ndiege, alisema ziara hiyo wilayani Sikonge imehitimisha rasmi mfululizo wa ziara za mafunzo kwa vitendo mkoani Tabora. Alibainisha kuwa jambo kubwa walilojifunza ni namna mkoa unavyotekeleza kwa vitendo sera na miongozo ya Serikali, hususan katika nyanja za uchumi, kijamii, kisiasa na kimazingira.
Aliongeza kuwa uzoefu walioupata utawasaidia washiriki wa kozi hiyo kuandaa taarifa na uchambuzi wa kina kuhusu utekelezaji wa sera hizo, na hatimaye kutoa ushauri mahsusi kwa Serikali katika maeneo mbalimbali waliyotembelea na kujifunza.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Sikonge, Mhe. Thomas Myinga, alisema wilaya hiyo imeupokea ugeni huo kwa furaha na fahari kubwa, akisisitiza kuwa maoni na ushauri uliotolewa na wataalamu hao, hususan katika maeneo ya matumizi ya ardhi,uwekezaji na viwanda, utafanyiwa kazi kwa lengo la kuongeza tija ya shughuli za kiuchumi na kuwanufaisha wananchi wa Sikonge na mkoa wa Tabora kwa ujumla.

Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa