Afisa Elimu Mkoa wa Tabora, Mwl. Upendo Rweyemamu, amefanya ziara ya ufuatiliaji wilayani Sikonge kwa lengo la kukagua hali ya utekelezaji wa shughuli za elimu na kuimarisha utendaji kazi katika ngazi mbalimbali za ufundishaji na ujifunzaji. Katika ziara hiyo, alikutana na Maafisa Elimu wa msingi na sekondari pamoja na wasaidizi wao, Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule za Sekondari, Walimu Wakuu wa shule za msingi pamoja na walimu wote wa ngazi hizo, ambapo alisisitiza umuhimu wa mshikamano na uwajibikaji katika kuboresha taaluma Sikonge.
Kupitia vikao hivyo, Mwl. Rweyemamu alipata fursa ya kusikiliza kero na changamoto zinazowakabili walimu, pamoja na kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ya elimu inayoendelea wilayani humo. Aidha, aliwahamasisha walimu na watendaji wa elimu kufanya kazi kwa bidii na kwa kuzingatia malengo yanayolenga matokeo makubwa na yenye tija kwa wanafunzi na jamii nzima kwa ujumla.
Ziara hiyo iliyokamilika kwa kutembelea tarafa za Sikonge na Kiwere,ilihusisha ufanyaji wa tathmini ya matokeo ya mitihani ya upimaji wa kitaifa ya mwaka 2025, ikiwemo Mtihani wa kumaliza elimu ya msingi, Mtihani wa upimaji wa kitaifa wa darasa la nne na upimaji wa kitaifa wa kidato cha pili, ambapo Afisa Elimu huyo alisisitiza matumizi ya takwimu hizo kama chombo cha kupanga mikakati ya kuboresha ufaulu. Alibainisha kuwa tathmini ya kina na usimamizi thabiti wa ufundishaji ni nguzo muhimu katika kufikia elimu bora na endelevu kwa Mkoa wa Tabora.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa