Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Paulo Chacha, amempokea Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, mkoani Tabora kwa ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa mkoani humo.
Awali akitoa taarifa ya maendeleo ya Mkoa wa Tabora, Katibu Tawala wa Mkoa, Dkt. John Mboya, amesema mkoa umeendelea kupata mafanikio makubwa katika sekta mbalimbali zikiwemo elimu, afya, miundombinu pamoja na eneo la ukusanyaji wa mapato. Kwa upande wa sekta ya elimu, Mkoa wa Tabora umefanikiwa kupata matokeo mazuri ya Kidato cha Sita kwa asilimia 99 na kushika nafasi ya pili kitaifa.
Katika sekta ya afya, Dkt. Mboya amesema Mkoa wa Tabora umefanikiwa kujenga hospitali za wilaya katika wilaya zote, pamoja na kuongeza vituo vya kutolea huduma za afya kutoka vituo 348 mwaka 2021/2022 hadi kufikia vituo 460 mwaka 2024/2025. Aidha, vituo vya kutoa huduma za upasuaji wa dharura kwa wajawazito vimeongezeka kutoka 25 mwaka 2021/2022 hadi kufikia 40 mwaka 2024/2025, sambamba na kuboreshwa kwa miundombinu ya kutolea huduma za afya ikiwemo Jengo la Wagonjwa Mahututi na Jengo la Wagonjwa wa Dharura.
Katika ziara hiyo, Mhe. Prof. Shemdoe alitembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa bwalo la chakula katika Shule ya Sekondari Tabora Wavulana unaogharimu shilingi milioni 200, mradi wa ujenzi wa barabara ya Mailitano yenye urefu wa kilomita 2.418 kwa kiwango cha lami, sehemu ya mradi wa TACTIC unaojumuisha jumla ya kilomita 10.7 kwa gharama ya shilingi bilioni 16.4, pamoja na mradi wa upanuzi wa Kituo cha Afya Mailitano unaogharimu shilingi milioni 675.
Baada ya kukagua miradi hiyo, Mhe. Prof. Shemdoe ameonesha kuridhishwa na utekelezaji wake na kutoa wito kwa wasimamizi kuhakikisha miradi inajengwa kwa viwango bora vinavyokidhi thamani ya fedha na kukamilishwa kwa wakati ili ianze kutoa huduma kwa wananchi. Aidha, amewaelekeza watendaji wa serikali kote nchini kuepuka matumizi yasiyo ya lazima na kuelekeza rasilimali zaidi kwenye miradi ya maendeleo ili kutimiza azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuwaletea wananchi maendeleo na ustawi.
Vilevile, Mhe. Prof. Shemdoe ameelekeza ujenzi wa miradi ya maendeleo uzingatie kikamilifu sheria na masharti ya mikataba, sambamba na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wakandarasi wazembe wanaochelewesha utekelezaji wa miradi, ikiwemo kuwakata sehemu ya fedha za malipo yao, kama ilivyofanyika kwa mkandarasi anayetekeleza mradi wa ujenzi wa barabara ya Mailitano.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa