Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Paulo Matiko Chacha, amewaongoza viongozi wa mkoa huo kuwapokea kwa shangwe wanamichezo waliouwakilisha mkoa katika mashindano ya UMISSETA ngazi ya Taifa yaliyofanyika mkoani Iringa kuanzia Juni 20 hadi 29, 2025.
Katika hafla hiyo maalum ya mapokezi, Mhe. Chacha aliwapongeza wanamichezo hao kwa ushindi mkubwa walioupata, ambapo Tabora ilishika nafasi ya tatu kitaifa kwa kupata alama 178.6, pamoja na kuibuka mabingwa wa kwanza kitaifa katika mchezo wa riadha.
Kwa upande wake, Afisa Elimu wa Mkoa wa Tabora, Mwalimu Upendo Ulaya, aliwashukuru kwa dhati viongozi wa serikali mkoa na wadau wote waliowezesha maandalizi ya timu hiyo. Alieleza kuwa, kwa mafanikio haya, tayari kuna mpango kabambe wa kuanzisha vitalu vya kuandaa vipaji vya wanamichezo mahiri kwa ajili ya mashindano umitashumta na umisseta kwa msimu ujao.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Dkt. John Mboya, hakubaki nyuma katika kupongeza juhudi hizo, akieleza kuwa ushindi huo ni matokeo ya kazi kubwa iliyofanywa na wachezaji, walimu na viongozi. “Ni fahari kwa Tabora, na ushindi huu umeendelea kutubakiza katika ramani ya michezo kitaifa. Endeleeni kuwa na nidhamu na kumcha Mungu katika kila hatua ya maisha yenu,” alisisitiza Dkt. Mboya.
Katika kuthamini mchango wa wanamichezo hao, Mhe. Chacha alikabidhi vyeti vya pongezi na zawadi kwa wachezaji na walimu wao, huku akidhamiria kuanza mchakato wa kuwachagua na kuwaendeleza vijana wenye umri chini ya miaka 17 watakaoweza kujiunga na timu za mkoa katika michezo mbalimbali.
Mashindano ya UMISSETA mwaka huu yaliandaliwa chini ya kaulimbiu: “Viongozi Bora ni Msingi wa Maendeleo ya Taaluma, Sanaa na Michezo — Shiriki Uchaguzi Mkuu 2025 kwa Amani na Utulivu.” Kaulimbiu hiyo ililenga kuhimiza ushiriki wa vijana katika maendeleo ya kitaifa kupitia taaluma na michezo sambamba na kuhamasisha mshikamano wakati wa uchaguzi mkuu ujao.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa