Mkuu wa wilaya ya Nzega, Mhe. Naitapwaki Tukai, ameongoza baraza la ushauri la mkoa (RCC) katika ukumbi wa mikutano wa Isike Mwanakiyungi, uliopo manispaa ya Tabora, kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Tabora, Mhe. Paul Chacha. Katika kikao hicho, katibu Tawala msaidizi, mipango na uratibu, Bw. Asanterabi Sang’enoi, aliwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mpango wa bajeti ya mwaka 2024/25 na mapendekezo ya bajeti kwa mwaka 2025/26.
Bw. Sang’enoi alisema kuwa, mkoa wa Tabora uliidhinishiwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kiasi cha shilingi bilioni 325.8, ambapo shilingi bilioni 314.5 ni kwa bajeti ya halmashauri, na shilingi bilioni 11.7 ni bajeti ya sekretarieti ya mkoa. Kwa mwaka wa fedha 2025/26, mkoa wa Tabora umepanga kutumia kiasi cha shilingi bilioni 367.2 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika mkoa huo.
Wajumbe wa mkutano huo walikubaliana kwa pamoja kupitisha rasimu ya bajeti ya mwaka 2025/26 na walipendekeza marekebisho yafanyike, hasa katika eneo la ununuzi wa magari ya viongozi na ujenzi wa ofisi za wakuu wa wilaya, maeneo ambayo walitaka yapatiwe kipaumbele.
Akichagia mjadala huo, Katibu Tawala wa mkoa wa Tabora, Dkt. John Mboya, alisisitiza umuhimu wa kuzingatia maelekezo mahususi katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka ujao. Alisema kuwa, ni muhimu kuepuka kuanzisha miradi mipya ya maendeleo kabla ya kumaliza miradi iliyopo. Aidha, alisisitiza kuwa ujenzi na uanzishwaji wa miradi ya maendeleo unategemea miongozo ya kitaalam kutoka katika wizara, na siyo matakwa ya viongozi wala wataalam wa maeneo husika.
Mwenyekiti wa kikao hicho, Mhe. Tukai, alitoa rai kwa viongozi na wananchi wa Tabora kushirikiana katika kutokomeza vitendo vya ukatili, ambao vimekuwa vikishamiri katika mkoa huu na hii ni kwa mujibu wa takwimu zilizowasilishwa na afisa ustawi wa jamii. Alihamasisha kuwa, kwa kushikamana, vitendo vya ukatili wa kijinsia vitakuwa historia katika mkoa wa Tabora.
Akifunga kikao hicho, Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Tabora, Ndg. Mohamed Nassoro Hamdan (MNEC), alishukuru kamati ya ulinzi na usalama mkoa wa Tabora, ikiongozwa na Mhe. Paul Chacha, kwa kazi nzuri ya kudumisha amani na utulivu. Alitoa wito kwa wananchi kuendelea kuitunza na kuidumisha amani hiyo, akisisitiza kuwa hakuna miradi ya maendeleo itakayoweza kuendeshwa wala kutekelezwa bila amani.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa