Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kanda ya Magharibi na Kati, Bi. Suma Atupele, ameongoza kikao cha tathmini ya utendaji kazi kwa mwaka 2024/2025 na kuwasilisha mpango kazi wa mwaka ujao wa 2025/2026, kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Bevac, ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Bi. Atupele amewataka wataalamu wa ununuzi wa umma kuwa wabunifu na kufanya kazi kwa bidii kubwa ili kufanikisha matarajio ya Serikali katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi. Amebainisha kuwa mafanikio katika sekta ya ununuzi wa umma yanategemea sana weledi, uwajibikaji na ufuatiliaji wa karibu wa shughuli zinazotekelezwa na taasisi za umma.
"Ni muhimu kuandaa na kuwasilisha mpango wa mafunzo kazini kwa wakati, huku tukizingatia uhalisia wa bajeti na utekelezaji wake ili kuongeza ufanisi na tija kazini," alisisitiza Bi. Atupele.
Ameongeza kuwa lengo la kuanzishwa kwa ofisi za kanda za PPRA ni kusogeza huduma karibu na wananchi na kufanya ukaguzi wenye tija unaolenga kuzuia upotevu, ubadhirifu na uharibifu wa fedha za umma katika utekelezaji wa shughuli za ununuzi kwenye taasisi za serikali.
“Ukaguzi tunaoufanya una lengo mahsusi la kuhakikisha kuwa fedha za Serikali zinatumika kwa uadilifu mkubwa na kwa manufaa ya wananchi,” alifafanua Meneja huyo.
Kikao hicho pia kiliambatana na mafunzo maalum juu ya majanga ya moto na ukoaji, yaliyoratibiwa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Tabora. Mafunzo hayo yaliongozwa na Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi hilo, Bi. Teresia Kipete, kwa kushirikiana na Koplo Stephano Kombo na S/Sgt Mayasa Choka.
Watumishi wa PPRA walipewa elimu juu ya aina za moto, visababishi vya ajali za moto, mbinu za kuzuia majanga hayo, pamoja na hatua za kuchukua pindi moto unapozuka katika majengo ya ofisi na makazi. Maafisa hao wamesisitiza umuhimu wa kuwa na vifaa vya kuzimia moto, kufunga ving’amua moto katika ofisi, kuwa na maeneo ya dharura ya mkusanyiko na mpango madhubuti wa kujinusuru wakati wa majanga.
Mafunzo hayo yamekusudia kuwajengea uwezo watumishi wa PPRA kanda ya Magharibi na Kati ili waweze kuchukua tahadhari na hatua stahiki kwa usalama wa maisha na mali pale wanapotekeleza majukumu yao ya kila.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa