Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi Dkt. Ally Posse amewataka wananchi wote kuchukua tahadhari kwenye makutano ya reli na barabara ili kuepukana na ajali ambazo zinaweza kuepukika. Ameyasema hayo leo Oktoba, 13 2023 alipokuwa akihitimisha maadhimisho ya Wiki ya Usalama wa Reli yaliofanyika kwenye viwanja vya Chuo cha Reli Manispaa ya Tabora.
“Tunapohitimisha Maadhimisho Ya Wiki Ya Usalama Wa Reli 2023, nawasihi wananchi wote kuendelea kuchukua tahadhari kwenye makutano ya reli na barabara ili kuepukana na ajali ambazo zinaweza kuepukika” alisema Dkt. Posse
Kufuatia uboreshwaji unaofanywa na Serikali ya awamu ya sita, Dkt. Ally amewasihi Watanzania kulinda miundombinu ya reli na kuwataka wanachi kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama ili kukabiriana na uharibifu huo.
“Niwasihi Watanzania wote tuwe walinzi wa miundombinu ya reli kwa maendeleo yetu sote na ukiona mtu au kundi la watu linahujumu miundombinu ya reli, huo ni uharifu, toa taarifa haraka kwa mamlaka za Serikali na jeshi la Polisi”Alisisitiza Dkt Ally.
Aidha, Naibu katibu Mkuu, ametoa wito kwa Watanzania kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hasa katika uwekezaji mkubwa unaofanywa kwenye sekta ya Reli na kukuza uchumi.
“Tuunge mkono juhudi za dhati za Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uwekezaji mkubwa unaondelea kwenye sekta ya reli na kukuza uchumi wa Tanzania” Alisisitiza Dkt. Posse
Maadhimisho ya Wiki ya Usalama yalizunduliwa na Mkuu wa wilaya ya Tabora Mhe. Peter Bura akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Balozi Dkt. Batilda Salha Burian, mnamo Oktoba 9, 2023 na kuhitimishwa leo na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi Dkt. Ally Posse Oktoba 13, 2023. Maadhimisho yenye kulenga utoaji wa elimu ya Usalama wa Reli kwa wananchi, yalienda sambamba na kauli mbiu isemayo “Usalama unaanza na wewe, Chukua tahadhari”
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa