Mganga Mkuu wa mkoa wa Tabora Dkt. Honoratha Rutanisibwa amefungua kikao kazi cha siku mbili kwa makatibu wa afya kutoka halmashauri zote za mkoa wa Tabora kinachofanyika katika ukumbi mdogo wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Tabora.
Awali akitoa neno la utangulizi, Katibu wa Afya mkoa wa Tabora Bw. Joseph Mwanambesi amesema lengo la kikao hicho ni kujengeana uwezo wa kiutendaji katika usimamizi wa mifumo ya afya katika vituo vya kutolea huduma za afya zinazojumuisha usimamizi wa rasilimali watu,usimamizi wa rasilimali fedha dawa na vifaa tiba,miundombinu,magari na mitambo.
Vilevile kuweka mikakati madhubuti ya pamoja ya namna ya kusimamia utekelezaji wa utoaji wa huduma katika vituo vya kutolea huduma za afya ndani ya mkoa wa Tabora,pamoja na kukamilisha kazi ya uandaaji wa taarifa za robo ya nne ya mwaka wa fedha 2024/25.
Katika hotuba yake ya ufunguzi, Dkt. Rutanisibwa aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuwekeza fedha nyingi katika sekta ya afya kwa lengo la kuboresha huduma katika ngazi zote. Alisisitiza kuwa uwekezaji huo mkubwa unahitaji kuendana na uwajibikaji wa hali ya juu kutoka kwa watoa huduma za afya katika zahanati,vituo vya afya na hospitali zote za mkoa wa Tabora.
“Wananchi wanategemea huduma bora zinazolingana na uwekezaji uliofanyika. Hivyo, ni wajibu wenu kuhakikisha watumishi walio chini yenu wanatoa huduma zenye staha, utu na weledi,” alieleza Dkt. Rutanisibwa.
Makatibu wa afya walioshiriki kikao hicho wameyapokea kwa moyo wa shukrani maelekezo yaliyotolewa, na kuahidi kuyafanyia kazi kikamilifu ili kuhakikisha maboresho ya huduma yanaonekana moja kwa moja kwa wananchi wa Tabora.
Kikao hicho kinatarajiwa kuibua mbinu bunifu za uongozi na usimamizi ndani ya sekta ya afya, na kuchochea mabadiliko chanya katika utoaji wa huduma kwenye vituo vya kutolea huduma mkoani humo.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa