Na Mwandishi Wetu – TABORA.
Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Mhe. Magdalena Rwebangira, amefungua rasmi mafunzo muhimu kwa waratibu na wasimamizi wa uchaguzi wa ngazi ya Jimbo, akisisitiza wajibu mkubwa walio nao katika kusimamia kwa haki na ufanisi mchakato wa uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.
Akizungumza katika ukumbi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Mtakatifu Augustino (AMUCTA) mkoani Tabora, Mhe. Rwebangira alieleza kuwa dhamana waliyopewa na Tume ya kusimamia uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ni nyeti, nzito na yenye athari kubwa kwa mustakabali wa demokrasia ya Tanzania.
Mhe. Rwebangira aliwakumbusha washiriki hao kuwa wanapaswa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo iliyowekwa kisheria na kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Alisisitiza umuhimu wa kushirikiana kwa ukaribu na vyama vya siasa pamoja na wadau wengine wa uchaguzi ili kuimarisha imani ya wananchi katika mchakato mzima wa uchaguzi.
“Epukeni kusababisha taharuki au malalamiko kwa vyama vya siasa.Hakikisheni mnazingatia ipasavyo Katiba,Sheria,Kanuni,Miongozo na maelekezo mbalimbali yaliyotolewa na yatakayotolewa na Tume,” aliongeza.
Mafunzo hayo ya siku tatu yanajumuisha jumla ya washiriki 110 kutoka mikoa ya Tabora na Kigoma, wakiwemo waratibu wa uchaguzi, wasimamizi wa uchaguzi ngazi ya jimbo, wasaidizi wao, maafisa wa uchaguzi, maafisa ununuzi na waratibu wa uchaguzi wa mikoa husika.
Kaulimbiu ya uchaguzi mkuu huo ni: “Kura Yako Haki Yako, Jitokeze Kupiga Kura”, kauli inayolenga kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika kuchagua viongozi wa ngazi zote kwa kutumia haki yao ya kikatiba.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa