MKUU wa Mkoa wa Tabora Dkt. Philemon Sengati ameagiza kuwachukulia hatua za kinidhamu kwa mujibu wa Sheria Watumishi wote waliopewa mashine za kukusanyia mapato (POS) ambao hadi hivi sasa wanadaiwa mapato waliyokusanya kwa kutowasilisha Benki.
Hatua hiyo itasaidia kuondoa na kuepuka dosari ya upotevu wa mapato ya Halmashauri ambayo inasababisha kuibuka Hoja za kiukaguzi kila mara.
Dkt. Sengati alisema hayo wakati akizundua Baraza jipya la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo.
Alisema Sheria ya fedha za umma inawataka Watumishi waliopewa mashine za kukusanyia mapato kuwasilisha fedha walizokusanya ndani ya saa 24 na sio vinginevyo.
Dkt.Sengati aliongeza kuwa ni marufuku kwa Wakurugenzi kuwaruhusu Wakusanyaji mapato kutoa asilimia yao(commission) kabla ya kuwalisha mapato Benki.
Alisema matumizi yoyote ya fedha kabla ya kuziwasilisha Benki ni kinyume na taratibu kwa kuwa Halmashauri husika haiwezi kutoa taarifa sahihi za makusanyo kimfumo.
“Naagiza kuanzia sasa ni marufuku kufanya matumizi ya fedha zilizokusanywa na Halmashauri kabla hazijapelekwa Benki” alisisitiza.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa aliwataka Madiwani kwa kushirikiana na Watendaji kubuni vyanzo vipya vya mapato kwa ajili ya kuiwezesha Halmashauri ya Urambo kuongeza mapato yake yatakayowawesha kujiendesha bila kutegemea ruzuku ya Serikali.
Alisema ni vema wakaanzia mashamba makubwa ya mazao mbadala na yale ya kimkakati kama vile mikorosho na miembe ili kuwavutia wawekezaji katika sekta ya usindikaji wa matunda.
Katika Baraza hilo limemchagua kwa asilimia 100, Adamu Malunkwi kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Urambo
Dkt. Sengati alisema hatua hiyo sio tu itaongeza mapato ya Halmashauri ya Wilaya ya Urambo bali itaongeza fursa za ajira kwa vijana.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa