Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Paulo Chacha, ameongoza uzinduzi wa mashindano ya michezo ya UMITASHUMTA na UMISSETA ngazi ya mkoa, katika hafla iliyofanyika Mei 19, 2025 katika viwanja vya michezo vya shule ya wavulana Tabora. Hafla hiyo ilihudhuriwa na wanamichezo, viongozi wa elimu, wadau wa maendeleo, walimu na wazazi kutoka halmashauri zote nane za mkoa wa Tabora.
Akimkaribisha mgeni rasmi, Katibu Tawala Msaidizi anayesimamia elimu, Bi. Upendo Rweyemamu, alimshukuru Mheshimiwa Chacha kwa kujitoa kwa dhati kuimarisha elimu na ustawi wa wanafunzi mkoani humo.
“Wewe ni mlezi wa kweli wa vijana wetu. Umekuwa mstari wa mbele kupambana na vitendo vyote vya ukatili dhidi ya watoto. Tunakuombea afya njema ili uendelee kuwa taa ya mkoa wetu,” alisema Bi. Rweyemamu.
Aidha, aliwashukuru wadau mbalimbali waliowezesha kufanikisha mashindano hayo, akiwataja Maafisa ElimuWilaya,Tapsha, Tahossa, Benki ya NMB, Umoja wa Maafisa Elimu Kata, na walimu wote kwa ujumla kwa ushirikiano wao wa hali na mali.
Katika hotuba yake, Mheshimiwa Chacha aliwapongeza wanamichezo wa UMITASHUMTA kwa kushika nafasi ya pili kitaifa kwa mwaka uliopita, akiwahimiza kuendeleza juhudi ili mkoa wa Tabora uibuke kidedea kwenye mashindano ya mwaka huu yatakayofanyika mkoani Iringa.
“Mimi nitafia barabarani kwa ajili ya kulinda ndoto za watoto. Tuwalinde watoto wetu dhidi ya ukatili wa aina yoyote. Tukiona dalili, tuchukue hatua. Tusiwafumbie macho wanaoleta madhara kwa watoto,” alisisitiza Mhe. Chacha.
Alitoa onyo kali kwa watu wasiowaheshimu watoto, akisema wazi: “Shuleni hakuna mwanamke, kuna watoto wa kike tu. Watoto wanapaswa kulindwa na kulelewa tu na wala si kutendewa vinginevyo.”
Aidha, aliwataka walimu wanaosimamia mashindano kuwa waadilifu na kuwatambua wanafunzi kwa vipaji vyao badala ya upendeleo:
Mashindano ya UMITASHUMTA yanayoshirikisha michezo kama mpira wa miguu,mikono, pete, wavu pamoja na sanaa za maonesho yamepangwa kufanyika kwa siku tano kuanzia Mei 17 hadi 22, 2025. Kwa upande wa mashindano ya UMISSETA, yatashika kasi kuanzia Juni 2 hadi Juni 6, 2025.
Zaidi ya wanafunzi 940 wanashiriki katika mashindano haya, wakiwemo wavulana 459, wasichana 481, na walimu, walezi pamoja na waratibu 97.
Mashindano haya yanaendeshwa chini ya usimamizi wa Wizara tatu: Wizara ya Ofisi ya Rais TAMISEMI, Elimu, na Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Mashindano hayo ya UMITASHUMTA NA UMISSETA yababebwa na Kauli mbiu ya mwaka huu isemayo “Viongozi Bora ni Msingi wa Maendeleo ya Taaluma, Sanaa na Michezo – Shiriki Uchaguzi Mkuu 2025 kwa Amani na Utulivu.”
.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa