MKUU wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt.Batilda Buriani ametegua kitendawili kilichodumu kwa kipindi cha miaka 9 cha kushindikana kufungwa kwa mashine ya kukoboa na kutenganisha mchele katika madaraja mbalimbali katika eneo la Mwamapuli wilayani Igunga.
Alisema haiwezekani mashine imenunuliwa mwaka 2013 kwa gharama ya milioni 30 hadi hivi sasa imeshindikana kufungwa kwa mvutano usio na msingi.
Balozi Dkt. Batilda ametoa uamuzi huo leo kwenye Mkutano Mkuu wa mwaka Ushirika wa Mwamapuli wilayani Igunga.
“Kama uongozi wa Halmashauri umeshindwa kulimaza mvutano huo mimi naagiza mashine ifungwe mara moja hapa Mwamapuli ili ianze kutoa huduma kwa wakulima wa vijiji vyote…kuendelea kuiacha kwenye stoo watu wanatushangaa na kutoona watu wa ajabu…miaka 9 mashine iko ndani vipuri vinazidi kuchakaa kwa kushindwa kufanya kazi” alisisitiza
Alisema vijiji vimeongeza kwa hiyo wazo la mashine imilikiwe na Kijiji kimoja halina maana tena ni vema ikafungwa katika Chama cha Ushirika ambapo itatoa huduma kwa wakulima wa vijiji vyote.
Balozi Dkt. Batilda alisisitiza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inataka mradi unapopelekwa kwa wananchi ufanye kazi kuwaondoa katika umaskini ndio maana Serikali imeendelea kutoa fedha nyingi kwa ajili ya uboreshaji wa sekta elimu, afya , miundombinu ya uchukuzi na huduma nyingine.
Katika hatua nyingine Balozi Dkt. Batilda aliigiza Kamati ya Usalama Wilaya ya Igunga kwa kushirikiana na Viongozi wa Ushirika wa Mwamapuli kuhakikisha wanawachukulia hatua kwa mujibu wa Sheria zilizopo wafugaji na wakulima wa mazao ya bustani wanaoharibu chanzo cha maji ya Bwawa la Mwamapuli.
Alisema watu hao hawatakiwi kufumbiwa macho kwa kuwa wanatishia uendelevu wa Bwawa hilo kwa kusababisha mchanga kuingia bwawani na kupunguza kina cha maji.
Mwanaushirika na Mwenyekiti Mstaafu wa Ushirika wa Mwamapuli Lazaro Ndulu alimuomba Mkuu wa Mkoa kuwasaidia kuwaondowa wafugaji ambao wanapeleka mifugo katika chanzo cha maji na kusababisha udongo kuingia bwawani kipindi mvua.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa