Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Balozi Dkt. Batilda Salha Burian amewataka maafisa mazingira Mkoani Tabora kuhahakikisha wanasimamia suala la usafi wa mazingira na ujenzi wa vyoo kwenye maeneo yote ili kupambana na magonjwa yatokanayo na uchafu. Ameyasema hayo leo Julai 28, 2023 wakati wa ufunguzi wa Kikao cha Tathmini ya Mkataba wa Lishe ngazi ya Mkoa, kwenye ukumbi wa Isike Mwanakiyungi.
Mkuu wa Mkoa alikili kuwa “Licha kuwepo mradi na kampeni za usafi wa mazingira katika maeneo mengi bado hali ya usafi wa mazingira na ujenzi wa vyoo katika kaya si ya kuridhisha, takwimu zinaonyesha uwepo wa vyoo bora kwa Mkoa wetu ni 75.8% hadi kufikia Juni 2023 na uwepo wa vyoo vya aina yoyote ni 99.6% na kaya ambazo hazina vyoo 0.4% na vifaa vya kunawia mikono kwa maji tiririka na sabuni ni 55%”.
Katika kuhakikisha Serikali inatoa lishe bora Kwa Wananchi, Dkt. Batilda amewataka Wakurugenzi wote Mkoani Tabora kutenga na kutoa fedha za lishe kama ilivyopangwa na Serikali kupitia wizara ya Afya.
“Nitoe rai kwa Halmashauri zote hususani Wakurugenzi kuzingatia maelekezo ya utengaji na utoaji wa fedha za Lishe kwa maana ya Tsh. 1,000 kwa kila mtoto mwenye umri chini ya miaka mitano na kuzitumia fedha hizi kwa shughuli husika.”
Aidha Mkuu wa Mkoa, amewapongeza Wakurugenzi kwa kusimamia na kutekeleza maazimio ya vikao vilivyopata na kuhakikisha bajeti zilizotengwa zimetekelezwa kwa mujibu wa maazimio yaliokubalika.
“Niwapongeze Wakurugenzi wote kwa kuboresha mipango na bajeti zenu baada ya kuwekeana maazimio hapa katika vikao vilivyopita vya tathmini ya mkataba wa lishe.”
Kikao hiki cha leo kinahusu mapitio ya Tathmini ya utekelezaji wa maazimio ya lishe ambayo yaliwekwa kwenye kikao cha awali ambacho maazimio yake yametekelezwa kwenye Halmashauri zote za Mkoa wa Tabora ambapo jumla ya Halmashauri nne (4) zilifanikiwa kukabidhiwa cheti cha utekelezaji wa maazimio hayo.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa